×

Rais Mteule William Ruto Afunguka “Mawaziri Wangu Watajibu Maswali Bungeni”

Rais Mteule wa Kenya, William Ruto.

Rais Mteule wa Kenya, William Ruto amesema kwamba mawaziri katika serikali yake watawajibishwa bungeni, kupitia kujibu masuali ya jinsi serikali yao inavyofanya kazi.

 

Vilevile William Ruto amewataka wafanyakazi wa umma kutoshiriki katika siasa na badala yake kuwahudumia wakenya wote bila kupendelea , chama, kabila au eneo wanalotoka

 

Akizungumza alipokutana na viongozi mbali mbali waliochaguliwa kupitia Muungano wa Kenya Kwanza, Ruto amesema kwamba watabadili sheria za vikao vya bunge kuhakikisha kwamba mawaziri wa serikali yake wanajibu masuali.

 

Amesema kwamba haitoshi kwa mawaziri kukutana na kamati za bunge pekee na kwamba ni muhimu waelezee wakenya jinsi serikali yao inavyowahudumia.

 

Amesema kwamba licha ya kuwa serikali yake itakuwa ya kidemokrasiani lazima iwajibike.

Kuhusu wafanyakazi wa Umma, Ruto amesema kwamba anawahakikishia kwamba kazi zao zipo salama na kwamba hawatahusishwa tena na masuala ya kisiasa kama ilivyo sasa.

 

Matamshi ya Ruto yanajiri siku mbili tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliopita ambapo matokeo yake yamezua mvutano katika ya tume ya uchaguzi nchini IEBC.

 

Siku ya Jumanne makamishna wanne wa tume ya uchaguzi IEBC kati ya saba walipinga matokeo yaliotolewa na mwenyekiti wao wafula Chebukati, wakidai kwamba yalikabiliwa na kiza kinene.

 

Makamishna hao wanadai kwamba hesabu ya matokeo iliotangazwa na Wafula Chebukati haiingiliana na jumla ya idadi ya kura ya wagombea wanne wa Urais.

 

Vilevile wanadai kwamba wafula Chebukati hakuwausisha katika kuhakiki matokeo ya mwisho kabla ya kuyatangaza kwa umma.

 

Tayari Aliyekuwa mpinzani mkuu wa William Ruto na waziri mkuu wa zamani Raila odinga ameapa kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo akisema kwamba mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alikiuka katiba kwa kutowahusisha makamishna wake katika mchakato wote wa kutangaza matokeo hayo.

Leave a Comment