
IMEFAHAMIKA kuwa, kiungo mpya wa Simba, Nassoro Kapama, amegoma kupunguziwa sehemu ya mshahara wake kikosini hapo wakati anajiunga na timu hiyo msimu huu.
Kapama ni kati ya wachezaji waliosajiliwa na Simba msimu huu akitokea Kagera Sugar, kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho ambacho kimepania kufanya kweli michuano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Kapama ambaye ni mchezaji kiaraka, amekataa kupunguziwa mshahara kutoka shilingi milioni nne hadi shilingi milioni moja ili atolewe kwa mkopo.
Mtoa taarifa huyo alisema mchezaji huyo yupo tayari kuondoka Simba, lakini kwa sharti la kutopunguziwa mshahara wake.
“Kapama hana shida, yupo tayari kwenda popote kwa mkopo, lakini kwa sharti la mshahara wake kutopunguzwa.
“Hiyo ni baada ya viongozi wa Simba kupanga kumtoa kwa mkopo na kumlipa mshahara wa shilingi milioni moja ambapo hajakubaliana na hilo,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Hilo suala ni la kiutendaji, hivyo tuwaachie wao ndio wanajua nani wa kumuacha au kumtoa kwa mkopo, hivi karibuni itajulikana.”
STORI; WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA