
KLABU ya mpira wa miguu kutoka nchini Uingereza,Bournemouth imemfuta kazi kocha wake Mkuu Scott Parker ikiwa ni mechi nne pekee ndani ya msimu mpya wa ligi kuu ya Uingereza.
Bournemouth wameachana na Parker, 41, baada ya kushindwa kwa mabao 9-0 dhidi ya Liverpool jumamosi iliyopita.

Baada ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa katika mechi ya kwanza ya msimu, timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu imepata vipigo vikali kutoka kwa Manchester City, Arsenal na Liverpool.
Na licha ya Parker kuwapandisha daraja kutoka ligi daraja la kwanza katika msimu wake wa kwanza wa kuinoa timu hiyo, mmiliki wa Bournemouth Maxim Denim amemtimua kocha huyo ikiwa ni katika jitihada za kuhakikisha klabu hiyo inaendelea huku wakiwa na matarajio ya kunusurika kwenye ligi kuu.

“Ningependa kutoa shukrani zangu kwa Scott na benchi lake la ufundi kwa jitihada zao wakati wao na sisi, kupanda kwetu daraja kurejea Ligi Kuu msimu uliopita chini ya uongozi wake kutakumbukwa daima kuwa moja ya misimu yenye mafanikio zaidi katika historia yetu”. Alisema Maxim
Aliendelea kwa kusema “Hata hivyo, ili tuweze kuendelea na maendeleo kama timu na klabu kwa ujumla, ni lazima tuwe sawa katika mkakati wetu wa kuiendesha klabu kwa uendelevu, pia tunapaswa kuaminiana na kuheshimiana. Hiyo ni mbinu ambayo imeiletea klabu hii mafanikio makubwa katika historia ya hivi karibuni, na ambayo hatutakengeuka kuanzia sasa. Utafutaji wetu wa kumtafuta kocha mkuu utaanza mara moja”
Imeandikwa na: John Mbwambo kwa msaada wa mitandao.