
LEO Septemba 1, 2022 Waziri wa Wizara Afya Mh. Ummy Mwalimu ametoa ufafanuzi juu ya kutetereka kwa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na kuweka wazi mipango ya serikali katika kuokoa mfuko huo ambao umeanza kuonekana kuzidiwa na changamoto zilizojitokeza.
Waziri Ummy ameweka wazi changamoto mbalimbali ambazo zinapelekea kuhatarisha utendaji kazi wa mfuko wa bima ikiwemo:
Idadi ndogo ya wachangiaji wa hiyari wa mfuko (wachangiaji wasiokuwa watumishi) huku wengi wao wakiwa ni wale waliolazimika kujiunga na mfuko huo kutokana na matatizo ya kiafya yanayo wakabili, hali hii hupelekea matumizi ya pesa kwenye mfuko kuwa makubwa kuliko kiasi cha uchangiaji.
Kukosekana kwa mifumo mizuri ya udhibiti wa watumiaji wa mfuko jambo linalopelekea matumizi mabaya ya kadi zao. Waziri alitoa mfano wa mgonjwa anayetumia kadi yake kupata matibabu kwenye hospitali mbili au zaidi tofauti kwa tatizo moja kabla ya kumaliza matibabu kwenye hospitali aliyoanza matibabu awali. Jambo hili linapelekea kusababisha matumizi makubwa yasiyo na ulazima hivyo kuurudisha nyuma mfuko.

Pia waziri alisema changamoto ya watumishi waliostaafu akisema kuwa mfuko unatumia gharama kubwa kuwahudumia baada ya kuustaafu na kulitaja kuwa moja ya jambo watakalo lishughulikia ili kuwahudumia vyema wakati huohuo kutoathiri mfuko.
Aidha waziri Ummy ameweka wazi mikakati ambayo serikali kupitia shirika la bima la taifa NHIF imejipanga kuitendea kazi ili kuuimarisha mfuko wa shirika la bima na kuhudumia wahitaji wote bila kutetereka ikiwemo:
Kuongeza idadi ya wachangiaji wa mfuko kwa kuweka sheria ya bima kwa watu wote ambayo itachochea uchangiaji na kuuokoa mfuko kwakuwa idadi kubwa ya wachangiaji hawatokuwa na matumizi makubwa ya bima zao.
Kuanza kutumia mifumo ya TEHAMA katika kudhibiti matumizi kwa wanachama wa mfuko ili kudhibiti matumizi mabaya ya kadi zao kama ilivyoelezwa kwenye changamoto alizozieleza.

Pia Waziri amesema kutakuwa na mkakati wa madaktari wa familia ambao kwa kiasi kikubwa unatarajiwa kupunguza mzigo kwa mfuko huo wa bima wa Taifa.
Waziri Ummy pia ametoa onyo kwa watoa huduma wanaofanya udanganifu kwenye amatumizi ya mfuko wa bima wa Taifa kwani hospitali za serikli na zile za binafsi zinategemea mapato kutoka katika mfiko wa bima wa taifa, hivyo hawatovumiliwa na hatua zitachukuliwa juu yao.
Mwisho Waziri Ummy amewahakikishia wanchama kuwa mfuko utaendelea kufanya kazi na waondoe hofu huku changamoto hizo zilizoonekana zikiendelea kuzishughulikia.
Imeandikwa: Abdallah Kaputi kwa msaada wa mitandao.