
MAKAMU wa Rais wa Argentina, Cristina Fernandez de Kirchner amenusurika kuuawa baada ya mwanaume mmoja kujaribu kumshambulia kwa risasi.
De Kirchner alishambuliwa baada ya kutoka nje ya nyumba yake na kuwasalimia wafuasi wake ndipo mwanaume huyo akajitokeza kwenye umati wa watu kisha kumnyooshea bunduki usoni.
Video zilizosambaa kwenye vyombo vya habari vya ndani ya nchi hiyo, zilionyesha mwanaume huyo akilenga bunduki inchi moja kutoka kichwani kwa kiongozi huyo.

Taarifa inaeleza kwamba de Kirchner yupo katika kesi ya ufisadi na alikuwa akirejea kutoka mahakamani lakini kiongozi huyo amekanusha madai hayo dhidi yake.
Rais wa Argentina, Alberto Fernandez alisema bunduki iliyotumika kutaka kumpiga kiongozi huyo ilikuwa na risasi tano na tayari uchunguzi unaendelea kwa ajili ya kubaini sababu ya shambulio hilo.

Rais Fernandez ameyasema hayo wakati akihutubia taifa Septemba Mosi, 2022 na kulaani shambulio hilo huku akitaja kuwa tukio hilo ni miongoni mwa matukio makubwa zaidi tangu nchi hiyo irejee kwa demokrasia mwaka 1983.

Polisi wa Argentina wamesema kwamba mwanaume huyo ambaye vyombo vya habari vya eneo hilo vilimtaja kuwa na umri wa miaka 35 raia wa Brazil tayari amewekwa mbaroni.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao