
EDOUARD Mendy amekataa ofa ya Chelsea ya ufunguzi wa mkataba mpya. Kipa huyo wa Senegal ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa mshahara mdogo zaidi katika kikosi cha Chelsea, lakini alikataa pendekezo la kwanza la mkataba mpya kwa sababu mshahara mdogo kuliko mlinda mlango namba mbili wa timu hiyo Kepa Arrizabalaga, ambaye analipwa pauni 190,000 kwa wiki.

Mkataba wa sasa wa Mendy uliotiwa saini alipojiunga kutoka Rennes Septemba 2020 utaendelea hadi 2025, na kocha mkuu Thomas Tuchel amesema Mendy ataendelea kuwa chaguo namba moja katika kikosi chake licha ya kuwa na makosa mengi yaliyoigharimu timu siku za hivi karibuni.

Tuchel alisema “Ni nafasi nyeti sana katika timu na inahitaji kujiamini na bahati ni nafasi ambayo wakifanya makosa kidogo tu, huadhibiwa”.
“Kwa upande wetu hali ni shwari. Tuna makipa wawili bora, vijana wawili wenye vipaji. Tunafahamu kwamba Mendy amekuwa na makosa mengi hivi karibuni lakini kwanza, tunashughulika ndani na kisha tutawaambia.”
Kikosi cha Tuchel kitamenyana na Dinamo Zagreb nchini Croatia katika mechi ya ufunguzi wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa leo.
Imeandikwa na:John Mbwambo kwa msaada wa mitandao