
BAADHI ya wafuasi wa ngome ya Raila Odinga iliyopo mjini Kisumu, wamesema wanatarajia kumuapisha Odinga kuwa Rais wa nchi hiyo ili Kenya iwe na Marais wawili na kwamba endapo watu hawataikubali hali hiyo wataomba Kenya igawanyike.
Mbali na kauli hiyo, pia wafuasi hao wamesema wanaikubali hukumu ya Mahakama ya Juu ya Kenya ya kutupilia mbali ombi la Odinga la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti, uliomtaja mpinzani wake William Ruto kuwa mshindi.

“Tutamuapisha Raila Amollo Odinga kuwa Rais mteule ili tuwe na marais wawili na iwapo lolote litatokea tutaitisha kujitenga ili Kenya igawanywe.”
Wafuasi hao wakati wakihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari wamesema kuwa wameikubali hukumu hiyo kwa kuwa wao ni wakongwe katika maisha ya nchi hiyo, wakidai kuwa tatizo kubwa linaloikumba nchi ya Kenya ni pesa wakimaniisha ‘Rushwa’

Odinga, amekuwa akifurahia uungwaji mkono wa hali ya juu, hasa kutoka maeneo ya magharibi mwa Kenya, na ameshindana zaidi ya mara tano katika chaguzi za Urais tangu 1997 na kila mara amekuwa akidai kudhulumiwa.
Imeandikwa na: Oswald Mwesiga kwa msaada wa mitandao.