×

Zaidi ya Watu 60 Wauawa Nchini Ethiopia, Ripoti ya Uchunguzi Imebainisha

Waombolezaji wakiomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao

ZAIDI ya watu 60 wameuawa na wengine 70 kujeruhiwa mwishoni mwa Agosti, mwaka huu katika eneo la Oromia ambalo ni kubwa na lenye watu wengi zaidi nchini Ethiopia.

 

Tume ya Haki za Kibinadamu nchini Ethiopia (EHRC) imetoa taarifa hiyo Septemba 5, 2022 na kueleza kuwa imepata taarifa hiyo kutoka kwa wakazi na maafisa wa eneo hilo.

 

Tume hiyo imesema kuwa katika mashambulizi ya siku mbili yaliyotokea kwenye maeneo hayo yalisababisha nyumba kuharibika na mifugo kuporwa.

Mauaji yanayosababishwa na ghasia nchini humo

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, zaidi ya watu 20,000 walikimbia  makazi yao kutokana na mashambulio hayo ambayo yalilenga maeneo kadhaa ya woreda na Wilaya ya Amru.

 

Mashambulizi mengine yalitokea katika eneo la utawala la Horo-Gudru kati ya Agosti 29 na 31, mwaka huu, ikiwa ni baada ya vikosi vya usalama kutumwa kwenda kwenye eneo hilo.

 

Aidha, tume hiyo imeonesha kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na watu wenye silaha kutoka maeneo ya Wilaya au Mkoa jirani wa Amhara, ikiwa ni baada ya kifo cha watu watatu wa jamii ya Amhara waliouawa na Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA), wakati wa operesheni ya kundi la waasi wa Oromo linaloendesha harakati zake katika eneo hilo.

Zaidi ya watu 20,000 wameripotiwa kukimbia makazi yao

Mkuu wa Mkoa huo amelishtaki kundi la OLA ambalo limekuwa likikabiliana na vikosi vya serikali tangu 2018, huku wakazi wawili wa eneo hilo  wakiwashutumu wapiganaji wa Amhara kwa kufanya mauaji hayo.

 

Mnamo Juni, 18 na Julai 4, mwaka huu wanakijiji 100 waliuawa na watu wenye silaha katika maeneo mawili ya Oromia Magharibi mwa nchi hiyo.

 

Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao

Leave a Comment