
TIMU ya mpira wa miguu kutoka Afrika Inland Church (AIC) Kongowe, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Bonanza la makanisa yote ya AICT Jimbo la Temeke, mara baada ya kuifunga timu ya AIC Mbande kwa bao 1-0.
Aidha wa upande wa Netiboli, timu ya wanawake kutoka katika Kanisa la AIC Chang’ombe ilifanikiwa kuibuka mabingwa wa mchezo huo mara baada ya kupata ushindi wa mabao 15-4 dhidi ya AIC Kigamboni.

Mbali na michezo hiyo miwili pia kulikuwa na michezo mingine mingi kama kukimbia na ndimu, kukimbia na gunia, riadha na shindano la kula huku yote yakifanyika kwa pande zote mbili kwa wasichana na wavulana.
Akizungumza na Championi Jumatatu mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa bonanza hilo, Mwenyekiti wa Idara ya Vijana Jimbo la Temeke, C.P.A Mayala Bubele, aliwapongeza vijana wote walioshiriki bonanza hilo huku akiamini kuwa vijana ndio msingi mkubwa wa kujenga imani kupitia michezo ambayo inatoa hamasa kwa urahisi na kuwapongeza mabingwa wote wa mashindano hayo.

“Kwanza nipende kuwashukuru vijana wote ambao tumeweza kukutana katika bonanza hili, pili niwapongeze washindi wote wa kila mchezo ambao wameshiriki, naamini wote walikuwa wanastahili kuwa washindi.
“Jambo lingine kwetu kama vijana tunatakiwa kuendeleza imani yetu kupitia michezo ambapo tunaamini vijana wengi wanapenda michezo, hivyo naamini baada ya kumalizika kwa bonanza hili, tutaandaa lingine bora zaidi ya hili, bado vijana tunaweza kufanya mambo makubwa,” alisema kiongozi huyo.
Na Marco Mzumbe