
HATIMAYE Kampuni ya utengenezaji mbolea ya SBL kutoka Kenya imeanza kugawa mbolea bure kwa wakulima wanaofika katika Viwanja vya Kimondo,Mlowo,Mbozi, mkoani Songwe.
Mkurugenzi Mkuu wa SBL Joe Kariuki amesema kwa kila mkulima atakayefika katika Banda la Kampuni ya Mbolea Tanzania TFC katika maonyesho ya Siku ya Mbolea Duniàni yanayofanyika kitaifa mkoani humo atapata mbolea hiyo bure kama alivyoahidi.

Leo wananchi walifurika katika banda hilo kugombea mbolea hiyo ambayo baadhi ya wananchi hao wameishukuru SBL kwa kugawa bure mbolea hiyo ili kuifanyia majaribio.
“Watengenezaji wengi wa mbolea nchini hawatupi wakulima ili tufanye majaribio hivyo mbolea nyingine zinakuwa hazifai lakini SBL wamefanya vyema kutupa bure” amesema Skin Mwakalobo.

Misululu mirefu ilitawala katika banda la TFC wananchi wakitaka kupata mbolea hiyo inayoelezwa kuleta tija kubwa nchini, Kenya. SBL imesema itaendelea kugawa mbolea hiyo bure kwa wakulima nchini kote na ambao watanunua mifuko zaidi ya mitatu watapata mfuko mmoja bure wa mbolea hiyo.
Mbolea hiyo inasambazwa na TFC nchini kote na imethibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA ambao ndiyo wandaaji wa maonyesho hayo. Mbolea hiyo ni organic ambayo imeelezwa kuwa rafiki wa mazingira hivyo kuleta tija katika sekta ya kilimo. Maonyesho hayo yaliyoanza Jana yatafungwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde.