Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware akielezea namna ambavyo Taasisi hiyo ilivyojipanga katika kusimamia shughuli za Bima hapa nchini ikiwemo Bima ya Afya kwa wote.
Serikali imesema kuwa kupitia utaratibu wa Bima ya afya kwa wote imejipanga kuhakikisha dawa, vifaa tiba vinapatikana vya kutosha huku watoa huduma wanaendelea kujengewa msingi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya, Edward Mbaga wakati wa semina kwa waandishi wa habari na Wahariri iliyolenga kuwaelimisha juu ya sheria ya bima ya afya kwa wote.
Mbaga alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani kupitia utaratibu huu wa bima ya Afya kwa wote, huduma za afya zinakwenda kuboreshwa kwa kuhaikisha dawa zinapatikana zakuboresha nakuongeza wataalamu na watoa huduma katika vituo vyote vya afya nchini.

“Tunafahamu kuwa kulikuwa na tatizo la baadhi ya wananchi waliojiunga na bima ya afya ikiwemo ya CHF wakienda kwenye vituo vya afya hawapati huduma au wanakosa dawa, nitumie fursa hii kuwaambia kwamba kupitia utaratibu huu Serikali imejipanga dawa zitapatikana za kutosha, wahudumu wetu wanaotoa huduma za afya nao tunaendelea kuwajengea misingi ili waweze kutoa huduma bora za afya, ” aisema Mbaga nakuongeza
“Mwananchi ukishajiunga na bima hii ya afya kwa wote unapata uhakika wa kupata matibabu wakati wowote unapougua hata kama huna fedha, pia utapata uhakika wa kupata huduma kuanzia ngazi ya zahanati mpaka ya taifa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kiwango hicho hicho ulichojiunga nacho,” alisema

Kuhusu utaratibu wa kulipia bima
Mbaga alisema kama sheria hiyo ya bima ya afya kwa wote itapitishwa na Bunge hakutakuwa na makundi makundi ya mafao ya bima na kwamba mtu akishajiunga kila kilichokuwa kwenye kitita cha msingi utakipata.
“Tupo katika hatua ya mjadala nakupokea maoni, ila viwango hivi vya uchangiaji uwa vinangawiwa kwa kuzingatia gharama halisi ya tiba na mahitaji halisi ya wananchi kwa maana ya afya,” alisema na kuongeza

“Kwa kuzingatia mahesabu na ili hospitali na vituo vya afya viweze kutoa huduma tumependekeza kiasi cha Sh. 340,000 kutolewa kwa kila kaya na kwa mtu mmoja ambaye hana familia atatakiwa kuchangia sh. 84,000, hii ni kwa kuanzia lakini nasisitiza bado tupo kwenye majadiliano,” alisema
Aidha alisema kwa mwananchi ambaye hatakuwa na uwezo wa kuchangia sh. 340,000 au 84,000 kwa mkupuo utaratibu utawekwa na TIRA ili kundi hilo liweze kuchangia na kupata fursa ya kupata bima kulingana na uwezo wa kipato chao.