
STAA wa zamani wa Manchester United, David Bekham anatajwa kuwa kwenye mpango wa kuinunua klabu hiyo katika mchakato ambao unatajwa kuwa na muunganiko wa wawekezaji ili kuongeza nafasi yao ya kushinda dili hilo baada ya familia ya Glazers kutangaza kuiweka sokoni.
The Glazers, ambao waliinunua Man United kwa pauni milioni 790 mwaka 2005, waliiweka sokoni klabu hiyo ya Old Trafford Jumanne ya wiki hii ambapo Gazeti la Mirror Football limeripoti kuwa wamepanga kuiuza kwa kiasi cha pauni bilioni 8.
Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa, uhusiano wa Beckham na mashabiki wa Manchester United unavutia uwezekano wa kufanyika dili hilo la Beckham ambaye aliwahi kuhusishwa miaka ya nyuma kutaka kuinunua United.

Katika mahojiano na Sky Sports mwezi Mei, Beckham alisema: “Kuna mabadiliko ya kufanywa, hakuna timu nyingi ambazo zimepitia yale ambayo wamepitia katika miaka michache iliyopita.”
Bilionea wa Uingereza na shabiki wa muda mrefu wa Man United, Sir Jim Ratcliffe aliweka wazi adhma yake ya kutaka kuinunua United na yuko tayari kutangaza dau lake baada ya jaribio la awali na lile la kuinunua Chelsea kushindikana.
Kufuatia taarifa hiyo umoja wa mashabiki wa Man United ulitoa taarifa iliyosema: “Katika miaka 17 iliyopita mashabiki wa Manchester United wamesikitishwa na umiliki wa klabu. Katika kipindi hicho tumeshuhudia kudorora kwa uchezaji na uwanja wetu. Lazima yawe mabadiliko sahihi. Kwa wakati huu, klabu yetu inahitaji uwekezaji mpya zaidi kuliko hapo awali.”