×

Mshambuliaji wa Singida Francis Kazadi Kasengu Awaita Yanga Mezani

Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Francis Kazadi Kasengu (mwenye rasta).

MSHAMBULIAJI wa Singida Big Stars, Francis Kazadi Kasengu, kwa mara ya kwanza ameweka wazi ishu ya Yanga kumuhitaji, huku akibainisha kwamba, yupo tayari kujiunga na timu hiyo endapo viongozi wa timu hiyo watamalizana na timu yake ya sasa, Singida Big Stars

Raia huyo wa DR Congo, amebainisha kwamba, tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Singida Big Stars kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, hivyo wale wanaosema hana mkataba, wanapotosha.

Kazadi ambaye juzi Jumapili alifunga mabao manne kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2023 dhidi ya Azam FC wakati Singida Big Stars ikishinda 4-1 na kufuzu fainali ya michuano hiyo, amekuwa gumzo kubwa baada ya kufanya hivyo.

Akizungumza na Spoti Xtra, Kazadi alisema kazi yake ni kucheza soka, hivyo kama Yanga wanamuhitaji, basi wanatakiwa kufanya haraka kuwasiliana na uongozi wa Singida, endapo watakubaliana, yeya hatakuwa na neno.

“Yanga kama wananitaka mimi sina neno, wanatakiwa kufanya mazungumzo na timu yangu ya Singida kwa kuwa ndiyo wananimiliki kwa sasa, hivyo kama watakubaliana nipo tayari kucheza kwao, waje fasta.

“Kuhusu mkataba wangu na Singida, nina mkataba wa miaka miwili, hivyo sipo hapa kwa majaribio, mimi kwa sasa ni mchezaji halali wa hii timu na ninafurahi kuona nimeanza kuwapa furaha kwa kufunga mabao muhimu,” alisema mchezaji huyo.

Kazadi ambaye amecheza mechi tatu za Kombe la Mapinduzi 2023 na kufunga mabao matano, kwa muda mrefu alikuwa akihusishwa na timu za Yanga na Simba kabla ya kuibukia Singida Big Stars.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 30, timu alizowahi kuzitumikia ni AS Vita Club, DC Motema Pembe, SCC Mohammédia, Wydad Casablanca na Al Masry.

STORI: MARCO MZUMBE

STRAIKA MKONGOMANI AZIGONGANISHA SIMBA NA YANGA, KAZADI AFUNGUKA ISHU YA YANGA | KROSI…

Leave a Comment