
“KAMA hakutakuwa na hali ya mvua katika Uwanja wa Manungu, basi tunaiomba Mtibwa Sugar isalimishe pointi zetu tatu mapema kabla ya dakika 90,” hiyo ni kauli ya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally akizungumzia mchezo wao ujao dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kesho Jumamosi.
Kesho Jumamosi, Simba itakuwa ugenini kuzisaka pointi tatu dhidi ya Mtibwa kwenye ligi kuu, huku wababe hao kutoka Msimbazi wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-0 kwenye mchezo wao uliopita.
Simba kwa sasa wako nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 54 baada ya kucheza mechi 23 ambapo wameshinda 16, sare sita na kupoteza miwili huku Mtibwa wakiwa nafasi ya tisa na alama zao 29 kupitia mechi 24 walizocheza na kati ya hizo wameshinda saba, sare nane na kupoteza 9.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ally alisema: “Kama hakutakuwa na hali ya mvua katika Uwanja wa Manungu, basi tunaiomba Mtibwa Sugar isalimishe pointi zetu tatu mapema kabla ya dakika 90 kuisha kwani tumejipanga kuvuna ushindi mapema zaidi.
“Tumeanza mazoezi leo (juzi Alhamisi) baada ya kuwa na mapumziko ya siku moja na taarifa ya kufurahisha hadi muda huu hatuna hata majeruhi mmoja, kwani wachezaji wetu kama Agustine Okrah na Ismail Sawadogo ambao walikuwa na majeraha tayari wamesharejea kikosini kuipambania timu,” alisema Ahmed.