ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Kwema kabisa,” nilimjibu nikikaa huku nikitamani kumwambia ukweli kuhusu hisia zangu kwake. Nilimpiga jicho moja la hasira, akaangalia pembeni na kusema:
“Kuna mwanamke mmoja jirani na wakwe zako kule kijijini hivi huwa mnaonana? Maana siku zile nilipokuja jamaa alinionesha. Sasa leo wakati nakuja hapa nimemuona pale kwenye kona ya dukani.”“Mh!” Niliguna kwanza.SASA ENDELEA:
“Ahaa! Wewe unasema unaitwa Tiaki kumbe ni Daniel,” nilijikuta nikisema kwa hasira huku nikimkazia macho.
“Nani anaitwa Daniel. Mimi niitwe Daniel halafu niseme naitwa Tiaki, kisa cha kukudanganya nini sasa? Angalia kitambulisho changu cha kazi,” alisema Tiaki huku akitoa hicho kitambulisho na kunionesha.
Nilikidaka, nikakiangalia. Kweli jina lake ni Tiaki lakini nikapata mshangao mwingine. Kampuni aliyokuwa akifanyia kazi Tiaki inaitwa PDM na mume wangu alikuwa bosi wa Kampuni ya PDM hivyohivyo ila nembo tofauti.
“Na wewe ulikuwa ukifanya kazi na marehemu baba Kisu?” nilimuuliza.
“Hapana.”
“Sasa mbona ni PDM? Mume wangu alikuwa bosi wa Kampuni ya Power Domestic Material.”
“PDM yangu hiyo ni ya Powell Domdom Meta.”
Niliishiwa nguvu zaidi. Moyoni nilikataa kwamba, haiwezekani kuwa na mambo yanayofanana kwa asilimia kubwa kati ya Tiaki na marehemu mume wangu, baba Kisu. Nilisema moyoni kuna kitu.
Niliamua kujiridhisha kwamba yeye siyo Daniel bali ni Tiaki huku nikijaribu kutafuta ushahidi mpya unaoonesha kuwa, yeye ni nani hasa kama si Tiaki.
“Kwa hiyo shemeji ulikuwa hujiamini siyo?” aliniuliza.
“Sikuamini. Unajua kuna mambo nimesikiasikia ndiyo yamenipa shida. Lakini naendelea kuchimba. Yaani wewe na mume wangu baba Kisu mmefanana kwa kila kitu.”
“Kumbe! Basi kama ni hivyo shemeji nafaa kuwa mrithi wake kwako,” alisema Tiaki kwa sauti iliyojaa shangwe na furaha.
Hilo la kuwa na shangwe peke yake lilitosha kabisa kuanza kujua Tiaki ni Daniel. Maana ndiye aliyetaka kunirithi kule kijijini. Lakini ni Daniel yule mwingine.
Nilicheka tu, sikumjibu kitu. Mara, Tiaki alisimama akiaga:
“Shemeji mimi sasa nakwenda. Tutaonana siku nyingine, nitakuja. Lakini kabla ya kuja nitakujulisha kwanza kwa njia ya simu.”
“Kwani una namba zangu za simu?” nilimuuliza haraka sana.
“Nikose tena shemeji. Jamaa alinipa. Siku moja alisema inaweza ikatokea ana shida kubwa na mimi halafu sipatikani, nitumie namba yako, akanipa.”
“Sawa shemeji, basi utanipigia wewe,” nilimwambia akiwa ameanza kutembea.
* * * *
Usiku wa siku hiyo, nililala nikiwa katika lindi la mawazo. Nilimfikiria sana Tiaki, nikamfikiria zaidi mume wangu marehemu baba Kisu lakini nilimuwazia pia wifi yangu. Sikujua nawaza nini hasa kuhusu hawa watu.
Mara, simu yangu iliita. Ilikuwa usiku wa kama saa nne hivi, nikatoka kitandani haraka kuifuata kwenye chaja ukutani.
Nilijua ni Tiaki lakini nilipoangalia ni wifi.
“Wifi kuna nini huko?” nilimuuliza kwa mshtuko.
“Huku kwema. Sasa nimeshangaa kaka Daniel alikuja nyumbani usiku huu, akasema hajawahi kusafiri na wala hana mpango wa kuja huko Dar. Sasa tumebaki tunaulizana na mama, kama kaka Daniel hajaja mjini, niliyemwona mimi ni nani?”
“Mh! Wifi hili suala lipo katika hatua mbaya sana. Sijui niseme nini? Wewe waja lini mjini wifi?”
“Nitakuja wiki ijayo.”
“Basi ukija tutaongea zaidi wifi.”
“Sawa.”
Baada ya kuagana na wifi, simu ilipigwa tena kabla sijafika kitandani, nikaipuuza. Nilijua wifi amesahau kuniambia jambo, nikasema nitampigia asubuhi.
Nilishindwa kulala, maana aliendelea kupiga na kupiga na kupiga. Ikabidi niende kuipokea. Hakuwa wifi ni namba ngeni kwangu. Moyoni nikasema sasa huyu atakuwa Tiaki.
Nilipokea.
“Haloo mama Kisu, mimi Tiaki. Nimepiga kwanza simu iko bize sana, nikaotea, nikajua unaongea na wifi yako kijijini. Pengine anataka kuja mjini sasa anaomba nauli,” alisema Tiaki kisha akacheka.
Akaendelea:
“Lakini nilitaka kukutakia usiku mwema shemeji yangu. Ila sasa, nataka kukwambia kitu kimoja. Lazima tukae na kuzungumza mimi na wewe. Unajua sina mke, sina chochote. Sasa nimeamua kuoa. Lakini kwa ninavyoona, mtu anayefaa ni wewe shemeji kwani naijua tabia yako ilivyo njema.
“Jamaa alikuwa akiniambia mambo mengi sana kuhusu wewe na mimi nakubali. Ndiyo maana nimeamua kusema waziwazi. Kama utakubali, nitakuvumilia uishi kwa kumwombeleza marehemu mpaka utakaposema sasa basi. Na mimi nitajichomoza kisheria sasa.
“Ila sasa kuna jambo moja shemeji. Wewe kuwa jasiri, usiyumbishwe. Achana kabisa na zile habari za yule shemeji yako wa kijijini, Daniel. Usimuwazie kabisa, we niwazie mimi tu.”
Palepale simu ilidondoka chini kutoka kwenye mkono wa kulia.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.