
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Afisa mtendaji mkuu wa timu ya soka ya Biashara United ya mkoani Mara Mariam Lima amewaomba wapenzi na mashabiki wa timu hiyo waliopo ndani ya mkoa huo na nje ya mkoa wa Mara kujitokeza kuichangia chochote timu hiyo ili isishuke daraja kutokana na kupitia kipindi kigumu hivi sasa.
Akizungumza na GlobalPublshers.co.tz Afisa mtendaji mkuu wa Biashara United Mariam Lima amesema “ni kweli kwamba Biashara united kwa sasa iko katika hali mbaya jambo ambalo inatakiwa wapenzi na mashabiki wa soka mkoani Mara wajitokeze kuinusuru ili isishushwe daraja maana tunapoelekea tutashindwa kupeleka timu uwanjani kucheza mechi ”
“Awali Kampuni ya Free Sports ndiyo waliopewa timu kwaajili ya kuiendesha lakini ghafla wameleta taarifa kwamba hawataweza tena kuiendesha timu hiyo jambo ambalo limeleta mpasuko mkubwa kwenye timu yetu baada ya wao kujiondoa klabu sasa haina hata chakula cha wachezaji, wachezaji wameanza kusambaa kurudi makwao jambo ambalo ni hatari kwenye timu yetu”
“Tunawaomba wadau na wapenzi wa soka wajitokeze kutusaidia kwanza tupate chakula cha wachezaji pili tupate fedha za kuwalipa wachezaji ili tumalize michezo mitano ambayo imebaki kabla ya ligi kumalizika na mimi niseme tunadaiwa Zaidi ya milioni 140 lakini tukipata chochote na tukaweza kusafiri tutakuwa tumeiokoa klabu hii” alisema
“Tumebakiwa na jumla ya michezo mitano kabla ya ligi kumalizika hivyo wadau watusaidie ili tuweze kumaliza ligi ili timu ya watu isishuke daraja, tumebakiza mchezo wa Pan African (HOME), Green Warrious (AWAY) Ndanda (home) Kengold (Away) Mbeya kwanza (Away) ukiangalia michezo yote hii inahitaji gharama hivyo tunawaomba wadau watusaidie timu iweze kumaliza ligi maana tukishindwa kupeleka timu uwanjani tutashushwa madaraja” alisema