
KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema anafurahishwa na ushirikiano uliopo kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo inayoongozwa na Henock Inonga.
Simba kwenye anga za kimataifa msimu huu hatua ya makundi baada ya kucheza mechi sita, ilitunguliwa mabao 7, robo fainali ya kwanza haijaruhusu bao.
Kituo kinachofuata ni dhidi ya Wydad Casablanca, mchezo unaotarajiwa kuchezwa kesho Ijumaa, Uwanja wa Mohamed V nchini Morocco ambapo matumaini ya wawakilishi hao wa Tanzania ni kufuzu nusu fainali.
Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema mpira ni mchezo wa makosa na wachezaji wamekuwa wakiimarika kila baada ya mchezo.
“Unaona kwenye upande wa ulinzi ninafurahishwa na namna wanavofanya kazi, mtazame Mohamed Hussein, Kapombe, (Shomari), Inonga (Henock) kila mmoja anafanya kazi kwa kujituma.
“Wote wanashirikiana na hii inaongeza nguvu kwenye eneo hilo kwani ili ushinde ni lazima uhakikishe kwamba haufungwi, hili ni jambo la msingi na tunalifanyia kazi kila wakati,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.
Inonga ambaye anafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Joash Onyango, jina lake limepenya kwenye kikosi bora cha CAF cha wiki baada ya kumalizika michezo ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
STORI: LUNYAMADZO MLYUKA