×

Penzi Kabla Ya Kifo-15

 

Msichana bilionea, Elizabeth Marcel anasafiri kwenda Morocco, huko, anakutana na mwanaume mzuri wa sura aitwaye Rasheed, anachanganyikiwa mno, ghafla anajikuta akianza kumpenda.SONGA NAYO

“Mbona unanishangaa hivyo?” aliuliza Rasheed huku akimwangalia Elizabeth kwa macho ya mshangao.
“Unaonekana tajiri sana!”
“Nani? Mimi? Hapana bwana! Mimi si tajiri,” alisema Rasheed huku akitoa tabasamu lililomuacha hoi Elizabeth.

“Hili ni jumba lako?”
“Ndiyo! Ni moja ya vibanda nilivyo navyo!”
“Vibanda? Nalo hili utaliita kibanda?”
“Ndiyo! Nisikilize Elizabeth, maisha yanaanzia mbali sana, nilitoka chini sana mpaka kuwa hapa,” alisema Rasheed.

“Na mimi ninataka kuwa tajiri kama wewe, nitaweza?”
“Hahaha! Elizabeth! Wewe ni bilionea, unataka kingine kipi?”
“Siri za kuwa trilionea!”
“Hahah! Mbona unajua kila kitu!”

“Hapana! Sijui vyote zaidi ya kujituma!”
“Sawa! Nitakufundisha, lakini kwanza tufanye kazi yetu. Nimekwishaanza kufanya matangazo juu ya mavazi yako, hakika utafanikiwa zaidi,” alisema Rasheed.
Walibaki na kuzungumza mambo mengi, kadiri alivyokuwa akimwangalia mwanaume huyo, Elizabeth alizidi kumpenda na kukiri kwamba hakuwahi kumuona mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama Rasheed.

Ilipofika saa tatu usiku, gari likamfuata na kisha kumchukua kumpeleka katika Hoteli ya Royal Sultan iliyokuwa katikati ya Jiji la Marrakech. Njiani, Elizabeth alikuwa na mawazo tele, bado alimfikiria mwanaume huyo ambaye alionekana kutokuwa na hisia zozote za kimapenzi juu yake.

Gari lilichukua dakika ishirini mpaka kufika katika hoteli hiyo ambapo alipoulizia ilikuwa ni ya nani, akaambiwa kwamba ilikuwa ni moja za hoteli za nyota saba zilizokuwa zikimilikiwa na Rasheed.

Elizabeth akazidi kuchanganyikiwa, wakati mwingine alijiona kama alikuwa ndotoni. Alikuwa bilionea mkubwa lakini kila alipoufikiria utajiri aliokuwa nao Rasheed, alijikuta akiwa maskini ambaye alihitajika kupambana sana mpaka kuwa tajiri kama alivyokuwa mwanaume huyo.

Akapelekwa mapokezi ambapo hapo akapewa ufunguo na kuelekea katika moja ya vyumba maalumu, VIP ambapo huko akatulia chumbani na kuanza kufikiria kuhusu mwanaume aliyekutana naye nchini hapo.

“Ni mwanaume mzuri sana, lakini nahisi natakiwa kupambana ili niwe zaidi ya hapa nilipo, huyu Rasheed asije kuwa kama Edson,” alisema Elizabeth wakati anazima taa na kulala.

Asubuhi ilipofika, akapigiwa simu kwamba tayari gari lilifika mahali hapo kwa ajili ya kumchukua, alichokifanya ni kwenda kuoga kisha kuvaa nguo zake na safari ya kuelekea nyumbani kwa Rasheed kuanza.

Alipofika huko, akaongozana na mwanaume huyo mpaka katika ukumbi ambao ulitarajiwa kufanyika uzinduzi wa mavazi yake kisha kuanza kuzungushwa huku na kule. Japokuwa siku hiyo haikuwa ya tukio kubwa lakini watu walijazana mahali hapo huku wengi wao wakiwa waandishi wa habari ambao walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.

“Ninajisikia faraja kuwa karibu na trilionea kama wewe,” alisema Elizabeth huku akimwangalia Rasheed usoni.

“Usijali, hata mimi nafurahi kuwa karibu na mtu anayejituma kama wewe, hakika unastahili kuwa ulipo,” alisema Rasheed.
Waliendelea kuzungumza huku wakionekana kuwa marafiki wa kipindi kirefu mno, Rasheed akamtoa Elizabeth mahali hapo na kumpeleka katika hoteli moja kubwa na ya kifahari kuliko zote nchini Morocco.

Huko ndipo alipokutana na mabilionea wengi wa Kiarabu. Kulikuwa na mkutano mkubwa uliohusu namna ya kuuinua uchumi wa Afrika kwa ujumla. Elizabeth alifurahia sana kukutana na watu hao ambao wengine alikuwa akiwasoma kwenye vyombo vya habari na kusikia taarifa zao tu, kukutana nao tu naye alijiona kuwa bilionea mkubwa.

“Ninafurahi kukutana nawe, wewe ni meneja wa kampuni ya mafuta ya Moroccan Oil Investment?” aliuliza Elizabeth, alikuwa akimuuliza mzee moja mwenye ndevu nyingi, aliitwa Bashir Baraak.

“Ndiyo! Wewe ni Elizabeth?”
“Ndiyo! Kumbe unanifahamu?”
“Mwanamke bilionea Afrika, kwa nini tusikufahamu! Nakukaribisha sana katika ulimwengu wa mabilionea,” alisema mzee Bashir huku akiachia tabasamu pana.

Kila mtu aliyemuona Elizabeth ndani ya jengo hilo alifurahia, alikuwa msichana bilionea aliyekuwa akiyaendesha maisha yake kupitia biashara zake mbalimbali. Kila alipokuwa akiwaangalia watu hao, hakuamini, hakujiona kustahili kuwa miongoni mwao mahali hapo.

“Unahitaji nini?’ aliuliza mzee Bashir, kikao kizima kilikuwa kimya.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo.

1 Comment

  1. kila kitu kinawezekana endapo mtu anijitambua nn anafanya, kujiamini,kupambana na kila changanoto, hakuna aliyezaliwa na pesa bali pesa hutafyutwa. kama ntu darasa la saba na anabiliki majumba ya kifaaari na pesa kibao ww je??????????? maisha ni akili. uweza mwanadada kuwa bilionea even tilionea.

Leave a Comment