
Bunge la Tanzania hatimaye limepitisha Azimio la kuridhia makubaliano ya ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na ile ya Umoja wa nchi za Falme ya Kiarabu UAE.
Makubaliano hayo yanalenga zaidi katika kuanzishwa ushrikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji wa maeneo ya bandari ya Dar es Salaam yatakayofanywa na kampuni ya Dubai ya DP World.
Kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo, mjadala mkali umeibuka bungeni humo ambapo baadhi ya wabunge wameoneesha wasiwasi wao wa Tanzania kuingia katika makubaliano hayo.
Mathalani, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee ni miongoni mwa waliooneesha wasiwasi na kusema ni majukumu ya mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) kuendeleza, kusimamia na kuendesha Bandari kwa mujibu wa Sheria ya Bandari ya mwaka 2014 ambayo ilifanyiwa maboresho mwaka 2019.
Kwa upande wake, Aida Kenani ambaye pia ni mbunge wa viti maalum, Chadema amesema jambo hili linataka mjadala mpana.
“Mheshimiwa Spika niseme kwamba, maamuzi yanayokwenda kufanyika, yatafanyika kwa niaba ya watanzania na ndiyo maana nasema hili jambo lilihitaji majadiliano mapana kwa maslahi ya taifa letu, ili watu ambao wanataka kutoa ushauri wao, na wenye hofu, waweze kuondolewa hofu zao,” amesema Aida.
Hata hivyo, akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa bungeni, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,8 Makame Mbarawa, amejaribu kuwatoa wasiwasi wabunge pamoja na watanzania kwa kusema uandaaji wa mikataba yote utasimamiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuongeza kuwa licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali bandarini, lakini bado ufanisi wake umekuwa ni mdogo huku changamoto kubwa ikiwa katika kitengo cha makasha kushindwa kuwekeza katika mitambo mikubwa.
Wakati hayo yakijiri nchini Tanzania, kumekuwa na mjadala mzito miongoni mwa wananchi na viongozi ambao wameonyesha hisia zao kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wengi wakisema hofu yao si Tanzania kuingia makubaliano na kampuni ya DP World, bali vipengele vinavyokubaliwa.
Bandari ya Dar es Salaam ni kitega uchumi muhimu kwa Tanzania huku ikiingizia nchi hiyo zaidi ya trilioni 7 katika mapato ya forodha.
Bandari ya Dar es Salaam inabakia kuwa kiunganishi muhimu cha biashara na mataifa yasiyo na bandari kama vile Zambia, Malawi, Uganda, Burundi Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo upande wa mashariki.
Hata hivyo, mshindani wake mkubwa ni Bandari ya Mombasa, Kenya ambayo nayo inaendeshwa na kampuni ya kigeni.