
Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka, ametembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwenye maonesho ya NaneNane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya nakuipongeza benki hiyo kwa kuwahudumia wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Frank Nyabundege alimwambia Katibu Mkuu Kiongozi kuwa TADB imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 608.5 ambayo imewanufaisha wakopaji 1,657,544.
Nyabundege alisema benki hiyo imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 800 kwaajili ya kusaidia mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (Building a Better Tomorrow – BBT) iliyo chini ya Wizara ya Kilimo. Pamoja na hayo, alisema kuwa benki imetenga shilingi bilioni 8 kama mkopo kwa vijana na wanawake ambazo zitakwenda kuwakopesha wahitimu wa mradi wa BBT kwa riba nafuu.
“TADB imetenga shilingi bilioni 8 kupitia program maalumu ya mikopo kwa wanawake na vijana, ambayo kwa kuanzia, benki itaanza kuwakopesha wahitimu wa BBT watakaofanya shughuli zao za kilimo kwenye shamba la vitalu, Chinangali, Dodoma,” alisema Nyabundege.
Kwa maelezo ya Nyabundege, mchango wa TADB katika kuwainua wanawake na vijana katika kilimo ni wa muhimu tukizingatia ya kwamba kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inasema “Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo ya usalama wachakula.”