
Zanzibar. Benki ya NCBA imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha uwekezaji wake kwenye sekta mbalimbali hususani ya utalii ili katika hatua inayolenga kukuza uchumi wa visiwani Zanzibar.
Benki hiyo imesema kuwa itaendeleza juhudi zake za kuzindua mifumo mipya ya kibunifu itakayochochea biashara na ushirikiano wake kati ya serikali na wateja wake kwa ujumla. Uimarishaji huu unaendana na dhamira ya NCBA ya kuhamasisha mabadiliko chanya na kuwezesha maendeleo endelevu katika jamii inayoihudumia.
‘Ninafuraha kuwatangazia kuwa tumeweka mikakati mipya ya kuwekeza katika sekta ya utalii Zanzibar. Huduma zetu zimebuniwa kwa kuzingatia mahitaji ya wateja wetu hasa wamiliki wa biashara katika sekta hii inayozidi kukua kwa kasi’, alisema Mkurugenzi Mkuu mpya wa NCBA Claver Serumaga alipokuwa akirejelea msimamo wa benki hiyo katika hafla ya chakula cha jioni na wateja iliyohudhuriwa pia na mgeni rasmi, Dk. Saada Mkuya, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar.

Msaidizi wa Mkurgenzi Mkuu, Julius Konyani akiwatambulisha baadhi ya wafanyakazi wa tawi la Visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi huyo aligusia mafanikio ya benki hiyo ya hivi karibuni katika kuendesha ushirikishwaji wa kifedha katika kanda hiyo. Alisema, ‘kupitia majukwaa kama M-Pawa inayotoa mikopo kwa wafanyabiashara na wajisiriamali, imefungua milango ya ushirikishwaji wa kifedha kwa zaidi ya Watanzania milioni saba. M-pawa imewawezesha wasiokuwa katika mfumo rasmi wa kibenki kubadilisha maisha yao’.
Waziri alipongeza hatua zinazochukuliwa na NCBA kuwasaidia Wazanzibari. Alifafanua, ‘Ningependa kuipongeza Benki ya NCBA Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika uchumi wetu wa ndani. Kupitia masuluhisho yao ya kibunifu ya kifedha, huduma za kimkakati, na uwezo wao mahiri, utawawezesha watu binafsi, wafanyabiashara na jamiiya Zanzibar kufikia kilele kipya cha mafanikio. Kwa kuboresha ikolojia unaokuza ujasiriamali, wanafungua milango ya fursa kwa wamiliki wa biashara, nakuleta hamasa ya uwezeshaji wa kiuchumi’.
Kama taasisi ya kifedha iliyobobea kwenye uvumbuzi, benki ya NCBA imeendelea kufanya vizuri baada ya kupata tuzo mnamo mwaka 2022 kama benki bora zaidi ya kidijitali nchini Tanzania. Benki hiyo imelenga kufanya uwekezaji zaidi ili kuchochea maendeleo nakuinua hali ya maisha kwa wateja wake na taifa zima kwa ujumla.