
MTENDAJI Mkuu wa Simba, Iman Kajula, ameibuka na kubainisha kwamba, wamekuja na mpango mkakati maalum msimu huu wa 2023/24 utakaowawezesha kubeba makombe yote waliyoyakosa katika misimu miwili mfululizo ambayo yalibebwa na Yanga.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya Simba kuwapoka Yanga kombe la kwanza la Ngao ya Jamii walilolichukua juzi Jumapili kwenye Fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Simba ilifanikiwa kubeba ubingwa huo kwa ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Yanga, baada ya dakika 90 kumaliza bila ya kufungana.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kajula amesema kombe lao la kwanza la Ngao ya Jamii walilolichukua ndiyo mwanzo, kwani katika msimu huu wamekuja na mpango maalum mkakati wa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ya ushindi kila mchezo utakaokuwepo mbele yao.

Kajula alisema kwa sasa nguvu na akili zao wamezielekeza katika ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi ili kuhakikiksha wanarejesha furaha ya mashabiki.
“Ni furaha kuona mpango mkakati maalum tuliouandaa viongozi wa kuhakikisha tunayarejesha makombe yote ya ndani katika msimu huu kuanza vizuri kwa kuchukua Ngao ya Jamii.
“Huo ndiyo mwanzo wa mpango wetu mkakati ambao tumeupanga uongozi, sasa hivi tunaelekeza nguvu katika ubingwa wa Ligi na Kombe la FA, msimu huu ninaamini ndio wenye mafanikio makubwa kwetu,” alisema Kajula.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alisema ahadi yake ya kuifunga Yanga, bado inaendelea na watafanya hivyo hadi atakapoondoka madarakani.
“Kama uongozi malengo yetu ni makubwa msimu huu, ikiwemo kuyarejesha makombe yote tuliyoyakosa katika misimu miwili iliyopita, tumeanza na Ngao ya Jamii, yanafuata mengine sambamba na kuendelea kuwafunga Yanga kila tutakapokutana nao,” alisema Mangungu.
STORI NA WILBERT MOLANDI