
Mamba aliyekuwa akiwashambulia watu na mifugo katika Kijiji cha Izindabo Kata ya Lugata Kisiwa cha Kome Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, amegeuzwa kitoweo na wananchi wa Kijiji cha Izindabo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema wamepongeza hatua ya serikali ya kuwagawia Kitoweo hicho ambacho kitawapatia afya njema.
Damumbaya Majani, mmoja kati ya wananchi waliomchuna mamba huyo kwa kushirikiana na maofisa wa Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (Tawiri), amesema nyama ya mamba ni lishe tosha na ni tiba mojawapo kwa magonjwa ya binadamu hasa wanaosumbuliwa na vidonda vya tumbo.
Oparesheni ya Vuna Mamba inayofanywa na maofisa wa Tawiri inalenga kuokoa maisha ya watu wanaofanya shughuli ndani ya Ziwa Victoria ambao wamekuwa wakiliwa na mamba ambao idadi yao imeongezeka.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Izindabo, Samwel Prosper ameongoza zoezi la wananchi wa Kijiji cha Izindabo kupata kitoweo hicho kwa kuzingatia ratiba walizojipangia ili kila anayehitaji kitoweo hicho apate.