
KOCHA wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameibuka na kutamka kuwa, Yanga ni bora kwa sasa kutokana kiwango bora ambacho wanachokionyesha.
Kauli hiyo imekuja hivi sasa mara baada ya timu hiyo, kutoka kupata ushindi mnono katika Ligi Kuu Bara ikitoka kuwafunga KMC FC na JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kila moja na Namungo 1-0.
Yanga pia juzi imetoka kuwafunga Al Merreikh ya nchini Sudan mabao 2-0 ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Kigali Pele huko nchini Rwanda ambako timu hiyo inautumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Katika msimu huu, Yanga imeonekana kuanza vema huku ikisifiwa na baadhi ya makocha kutokana na ubora wao wanaouonyesha.

Akizungumza na moja ya kituo kikubwa cha radio Bongo, Julio alisifu ubora wa kikosi cha Yanga katika msimu huu kutokana na kiwango wanachoendelea kukionyesha katika ligi na kimataifa.
Julio alisema kuwa, ubora huo wa Yanga umetokana na kukaa pamoja muda mrefu juku wakiingiza maingizo machache ya wachezaji katika msimu huu ambao wameongeza chachu ya ushindi.
“Yanga wanacheza vizuri kwa sababu wamekaa pamoja muda mrefu na wameingiza watu wachache ambao wamekuja kuleta chachu timu ifanye vizuri katika msimu huu.
“Kikubwa mashabiki wa Yanga, wanatakiwa kumpa muda zaidi kocha kuandaa timu yake, ninaamini watafanya vizuri zaidi katika msimu huu.
“Napongeza usajili mkubwa ambao wameufanya katika msimu huu, ambao umeleta hali ya kila mchezaji kupambania namba,” alisema Julio.