×

Yanga Yakubali Kipigo Mbele Ya Ihefu Kwa Mara Nyingine Kwenye Dimba La Highland Estate – Video

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi, amekaribishwa kwenye Ligi Kuu Bara rasmi baada ya jana kushuhudia kikosi chake kikikandwa na Ihefu mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.

Katika mchezo huo, Gamondi mrithi wa mikoba ya Nasreddine Nabi, alianza kushuhudia timu yake ikifunga bao la mapema likifungwa na Pacome Zouzoua dakika ya tatu akitumia pasi ya Clement Mzize.

Ihefu chini ya Kocha, Zuberi Katwila, ilisubiri mpaka dakika ya 40 kupachika bao la kusawazisha kupitia kwa Lenny Kissu aliyemalizia mpira uliookolewa na kipa, Djigui Diarra.

Dakika 45 za mwanzo, zilikamilika kwa wababe hao kutoshana nguvu ya sare ya bao 1-1.

Charles Ilanfya, alipachika bao la ushindi kwa Ihefu kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa dakika ya 67 ambapo lilidumu mpaka dakika 90 zilipokamilika na ubao kusoma Ihefu 2-1 Yanga.

Ihefu inaendeleza rekodi yake ya msimu wa 2022/23 ilipowafunga Yanga kwenye mchezo wa ligi uliochezwa uwanjani hapo kwa mabao 2-1 na kuvunja rekodi ya timu hiyo kucheza mechi 49 mfululizo za ligi bila ya kupoteza.

Kipigo cha jana, ni mchezo wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu Yanga inapoteza kati ya minne kwa kuwa mitatu ilishinda na ilikuwa haijfungwa bao hata moja. Jana Djigui Diarra aliokota mabao mawili kwenye nyavu.

Leave a Comment