ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Sawasawa, aingie tu,” alikubali baba Pilima…
“Ee mama Pilima mpenzi wangu…geti kubwa..? Oke…sasa ingia ndani basi, ukiingia tu utaniona nimekaa na jamaa yangu mmoja ni mfanyabiashara,” alifunguka baba Pili.
SHUKA NAYO SASA…
Baba Pili akakata simu haraka, kisha akawa anaangalia geti kuu wanaloingilia wateja akiamini mama Pilima ataingia muda huohuo ili ampe ishara kuwa, yeye amekaa palepale.
Mara, uso wa baba Pili ambaye alipokaa alikuwa akiangalia geti kuu, ulionekana kujaa tabasamu laini kuashiria kwamba, mgeni aliyemtarajia, sasa alikuwa anaingia ndani ya ukumbi huo wenye kukusanya watu wengine jijini Dar.
Mama Pilima alitangulia kumwona baba Pili kwani alipokaa uso wake ulikuwa dhahiri, lakini hakumwona mumewe aliyekaa kwa vile mgongo ndiyo uliangalia getini.
Mpaka anafika pale, alikuwa hajamtambua mumewe, hasa kutokana na mkao wake wa kuinamia meza. Inaonekana baba Pilima aliamua kukaa hivyo ili asigundulike haraka.
Mama Pilima, akiwa na uso uliojaa tabasamu la kujua anavuta mkwanja aliouomba, alianza kupeleka mkono kwa baba Pilima kwanza huku akisalimia kwa sauti yenye bashasha, tamu, ya kumtoa nyoka kwenye shimo lake…
“Mambo baby wa miye?”
“Poapoa, karibu sana mpenzi wangu…”
“Oke asante sweet,” alisema kisha akaachana na mkono wa mwenyeji wake huyo na kupeleka mkono kwenye mkono wa mumewe…
“Mambo anko?”
Mumewe aligeuka kiufasaha na kumwangalia mama Pilima usoni ili amwone sawasawa…
“Haaa!” alishtuka mama Pilima.
Mwili wote ulimwisha nguvu, akahisi kizunguzungu, akaanguka chini…puu! Mkoba kule, viatu huko!
“Bwana Emmanuel vipi tena? Mbona huyu mgeni wangu alipokuona wewe tu amepatwa na mshtuko?” aliuliza baba Pili huku akimtumbulia macho baba Pilima…
“Hata mimi sijui, aulizwe yeye, labda amenifananisha.”
Wateja wa baa hiyo walianza kujaa wakimzunguka mwanamke huyo, wengine wakisema ameshafariki dunia, wengine amezimia tu. Wapo waliobashiri kuwa, lazima mgeni wa baba Pili atakuwa anajuana naye tu.
Baba Pilima alitulia kimya akijifanya kweli hajui lolote lakini akimwangalia mkewe kwa macho yaliyojaa mshangao na kujikaza jambo f’lani la ndani sana!
Huduma ya kwanza ilitembea, watu wakatakiwa kukaa pembeni ili mwanamke huyo apate upepo kwa maana ye hewa safi ya oksijeni.
Baada ya dakika kumi na tano hivi, mama Pilima alishtuka. Kijasho chembamba kikimtoka. Alianza kwa kufumbua macho kwa kupepesapepesa huku akiendelea kulala kisha baadaye, akakaa.
Baada ya muda, baba Pili akamsaidia kumkalisha kwenye kiti huku akimpa pole nyingi au tuseme za kumwaga. Si mpenzi wake, sasa je?
“Mama Pilima,” aliita baba Pili kwa sauti ya kumdekeza aliyemwita.
Mama Pilima alikuwa amejiinamia tu kwenye meza. Muda huo, uso wake ulikuwa bado una aibu maana alitambua kwa nini alianguka na kuzimia. Mkoba wake na viatu vyake viliwekwa katika hali ya usalama…
“Mama Pilima,” aliita tena baba Pili, safari hii kwa sauti ya kubembeleza…
“Abee…”
“Pole sana…”
“Asante.”
“Pole sana,” safari hii alisema baba Pilima.
“Asante,” mama Pilima, bila aibu wala soni, achilia mbali haya, eti aliitikia pole ya mumewe…mh!
“Kwani ulijisikiaje?” aliuliza baba Pili.
Kabla mama Pilima hajajieleza, baba Pilima akadakia…
“Bwana Mutu…”
“Naam bwana Emmanuel…”
“Mimi nadhani acha niende, shemeji akiwa ametengemaa, nipigie simu nikuletee mzigo mahali popote pale utakapokuwa…”
“Bwana Emmanuel naweza kukuruhusu, nitakujulisha kila kitu,” alisema baba Pili huku baba Pilima akisimama na kuondoka zake…
“Pole sana,” alimpa pole nyingine mke wake na kuanza kutembea.
Nyuma sasa, baada ya kupita kama dakika tano nzima bila kuwepo wa kuongea, ukimya ulikatika…
“Mama Pilima…”
“Abee…”
“Ni nini kwani mpenzi wangu?”
Mama Pilima kabla hajajibu, aligeuka kuangalia geti kuu, nadhani kujiridhisha kama mumewe alishaondoka kabisa eneo lile…
“Baba Pili, unamjua yule?”
“Eee…anaitwa Emmanuel.”
Mama Pilima alitingisha kichwa cha kukataa kwamba, yule si Emmanuel…
“Yule anaitwa Marco…”
“Marco? We unamjua? Au umemfananisha?”
“Namjua…”
“Ni nani?”
Kabla mama Pilima hajafunguka simu ya baba Pili iliita, aliyepiga ni baba Pilima kwani aliseviwa kwa jina la Emmanuel…
“Subiri kwanza nimsikie huyu mgeni aliyeoondoka,” aliomba baba Pili…
“Haloo bwana Emmanuel…”
“Mimi si Emmanuel, naitwa Marco au baba Pilima…”
Je, unajua nini kilitokea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.