
Wabunge 17 wa upinzani nchini Zambia wamezuiliwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa siku 30, kufuatia kuvurugu zilizokumba bunge hilo wiki iliyopita.
Wabunge hao walikaidi amri ya kuondoka kwenye kikao hicho baada ya kumshutumu Spika kwa kuwanyima fursa ya kuzungumza.
Akiwasimamisha kazi siku ya Jumanne, Spika Nelly Mutti alitaja mienendo ya wabunge hao kuwa isiyo ya kibunge na ukiukaji wa heshima na uadilifu wa Bunge.
Bi Mutti alisema kuwa uvunjaji wa sheria haupaswi kuchanganyikiwa na uhuru wa kujieleza na kumkaidi Spika ni sawa na kushambulia demokrasia ya kikatiba ya Zambia.
Mbunge Brian Mundubile, kiongozi wa upinzani bungeni, alikuwa miongoni mwa waliosimamishwa kazi.
Wabunge hao wanadai chama tawala kinataka kushinikiza baadhi ya mabadiliko ya katiba bila kuwepo.
Baadhi ya wabunge wa upinzani wameripotiwa kuwasilisha ombi la kuondolewa kwa Spika kwa madai ya usimamizi mbaya wa masuala ya bunge.