×

Azania Na TIC Watia Saini Makubaliano Ya Kushirikiana

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Gilead Teri (kulia) na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Benki ya Azania Bw. Charles Mugila (kushoto) wakitia saini makubaliano ya kushirikiana baina ya taasisi hizo mbili yenye lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na kituo cha TIC kupitia uzoefu wa Benki ya Azania katika kutoa huduma ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kituo hicho katika kuboresha huduma zake na kuongeza ufanisi na kuwavutia wawekezaji wengi Zaidi. Hafla ya utiaji saini imefanyika jana katika ofisi za kituo hicho jijini Dsm.

Benki ya Azania na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wametia saini makubaliano ya kushirikiana ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kituo cha Uwekezaji katika kuboresha huduma zake na kuongeza ufanisi lengo likiwa ni kuwavutia wawekezaji wengi Zaidi kuja kuwekeza nchini.

Akiongea katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika katika ofisi za kituo hicho jijini Dsm, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Gilead Teri alisema kuwa kituo hicho kinayo furaha kuingia makubaliano ya kushirikiana na Benki ya Azania kwa kuwa ni Benki pekee ambayo imeonesha uwezo mkubwa wa kiutendaji,

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Benki ya Azania Bw. Charles Mugila (kushoto) akielezea lengo na ushirikiano huo.

‘’Sisi kama TIC tunaamini kuwa ili tuweze kuongeza ufanisi katika kuwahudumua wawekezaji wa nje na ndani, ni vyema tukashirikiana na wadau ambao wana uzoefu na uwezo kutuzidi, na ni wazi kuwa Benki ya Azania kwa sasa wameonesha uwezo mkubwa katika hilo hivyo tunaamini kupitia makubaliano haya sisi kama kituo tutafaidika vilivyo katika kuboresha mifumo yetu, kuboresha huduma zetu na kuweza kuwahudumia wawekezaji kwa weledi zaidi, You can only see further if you stand on the shoulders of the Giants’, alimalizia Bw. Teri.

Naye Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Benki ya Azania Bw. Charles Mugila alisema kuwa Benki hiyo inaamini kwa kupitia makubaliano haya ya kushirikiana na kituo cha Uwekezaji, Wawekezaji wengi Zaidi watavutiwa na hivyo kuchangia katika kutoa fursa Zaidi za ajira na ongezeko la ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa ujumla.

Leave a Comment