
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema Desemba 30, 2023 kitafanyika kikao maalum kwa Wakuu wa Mikoa kujieleza kwa Rais kuhusu ujenzi wa shule zote kwenye maeneo yao.
Shule hizo zinajengwa kupitia Mradi wa uboreshaji elimu ya awali na msingi (BOOST) na wa elimu ya sekondari (SEQUIP).
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Mchengerwa amesema Rais aliwaamini walimu na kuwapa jukumu la kusimamia miradi hiyo ya elimu.
Amesema kwenye mradi wa SEQUIP imefanya vizuri lakini yapo maeneo hayajafanya vizuri kutokana na
changamoto mbalimbali.

“kwa taarifa nilizonazo katika miradi hii mradi wa shule karibu 229 yapo maeneo tumefanya vizuri na kuna maeneo ujenzi wa shule saba mpaka leo hawajaanza.”amesema Mhe. Mchengerwa.
“Yapo maeneo ndo kwanza wapo kwenye msingi na tunafungua shule januari, yapo maeneo kuna maboma hatujamaliza, yapo maeneo karibu shule 184 wapo kwenye hatua nzuri ya umaliziaji, nyingine zipo
kwenye msingi ambazo ni shule 10 na zilizokamilika ni 18.”

Amesema wakati Serikali inatekeleza miradi ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari ni kutokana na maono ya Rais miradi hii alifikiri yeye alitafuta fedha ndani na nje ya nchi ipo miradi ya SEQUIP, BOOST, EP4R, GPE, Shule Bora na mingineyo.
Amesema pamoja na jitihada hizo wapo miongoni mwao wameshindwa kumaliza baadhi ya shule hizo kutokana na kuingiliwa majukumu na Wakurugenzi na viongozi wakubwa wa serikali.
“Wapo Wakurugenzi ambao walikuwa wanawaingilia kwenye maeneo yenu, wapo wakurugenzi wa halmashauri tuliwakabidhi nyenzo na fedha za kufanya kazi nyinyi walimu kusimamia baadhi ya miradi lakini baadhi ya watendaji wa serikali wengine viongozi wakubwa kwenye serikali wamewaingilia.”
“Hali iliyopelekea hadi leo hii shule saba hazijaanza na fedha zimetolewa muda mrefu na wengine wapo kwenye maboma, wengine msingi nimeshawaelekeza wakuu wa mikoa Desemba 30 nitafanya nao kikao popote watakapokuwa ili wanipe taarifa ya utekelezaji wa agizo hili ili ifikapo tarehe 31 shule zote ziwe zimekamilika.