
Tshisekedi alipata asilimia 73.47 ya kura wakati wa uchaguzi wa Desemba 20 mahakama ya katiba DRC imesema.
Mahakama ya katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imethibitisha ushindi wa kishindo wa Rais Felix Tshisekedi katika uchaguzi wa mwezi Desemba kwa ajili ya awamu ya pili madarakani katika taifa hilo maskini, lakini lenye utajiri mkubwa wa madini katika eneo la Afrika ya kati.
Tshisekedi alipata asilimia 73.47 ya kura wakati wa uchaguzi wa Desemba 20, mahakama imesema. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilifanya uchaguzi wa rais, wabunge, majimbo na serikali za mitaa hapo Desemba 20 ambao viongozi wa upinzani waliuita “ni wa aibu”.
Wagombea tisa wa upinzani walitia saini tamko mwishoni mwa mwezi Desemba wakikataa kile walichokiita uchaguzi wa aibu na kutaka uchaguzi urudiwe. Zaidi ya watu milioni 40 kati ya wakaazi milioni 100 wa nchi hiyo kubwa waliandikishwa kupiga kura Desemba 20 kwa kiti cha rais, wabunge wa kitaifa na wa majimbo, pamoja na madiwani wa manispaa.