Bilionea mwanamke Afrika, Elizabeth Marcel anasafiri kwenda nchini Morocco kuzindua mavazi yake aliyobuni, anapofika huko, anakutana na mwanaume Rasheed ambaye anatokea kuuteka moyo wake, akawa hali wala halali kwa kumuwaza.
SONGA NAYO…
“Najua ni ngumu ila unatakiwa ufanye hivyo! Watu wengi wamepoteza wateja kwa kuwa walikuwa na hasira sehemu za kufanyia biashara na mwisho wa siku wanawajibu vibaya wateja, ifanye biashara yako ivutie, ifanye biashara yako iwe bora siku zote na kitu kinachoweza kufanya hivyo ni tabasamu lako pana,” alisema Noah.
“Sawa! Nitafanya hivyo! Ningependa nifahamu mengine.”
“Jishushe,” aliingilia tajiri mwingine, huyu aliitwa Thomas Khone kutoka Afrika Kusini.
“Kivipi?”
“Unatakiwa kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu pasipo kujali kama mtu huyo ni mkubwa, mdogo, maskini au tajiri,” alisema Khone huku akimwangalia Elizabeth machoni.
Siku hiyo ilikuwa ni siku pekee ya kufundishwa namna ya kuwa trilionea mkubwa katika maisha yake, baada ya kupewa njia za kutajirika zaidi, hapo ndipo akaondoka na Rasheed kurudi hotelini.
Alitamani mwanaume huyo azungumze neno lolote la mapenzi au hata kumuonesha ishara fulani lakini hilo halikufanyika, kila neno alilolizungumza mwanaume huyo lilionesha ni jinsi gani alithamini fedha kuliko mapenzi.
“Ungependa kupata nini katika maisha yako?” aliuliza Rasheed.
“Ninatamani kuwa na vingi mno, ila ninahitaji kitu kimoja zaidi,” alijibu Elizabeth.
“Kipi?”
“Mtoto!”
“Kwani huna mtoto?”
“Sina, sijabahatika kuwa naye!”
“Mungu wangu! Pole sana! Na mumeo anasemaje?”
“Sina mume.”
Waliendelea kuzungumza mengi, baada ya kufika hotelini, Rasheed hakutaka kubaki hapo, alichokifanya ni kuondoka kurudi nyumbani kwake huku akimwambia Elizabeth kwamba kesho yake wangezungumza mengi zaidi.
“Rasheed ananitesa,” alisema Elizabeth huku akilivuta shuka lake kwa ajili ya kulala lakini bahati mbaya kwake usingizi haukupatikana kirahisi mpaka ilipofika saa sita usiku ndipo alipolala.
Siku ambayo waliitarajia ikafika, watu wengi walikuwa wamekusanyika katika ukumbi uliotarajiwa kufanyika kwa uzinduzi wa mavazi hayo, kila mtu aliyeziona picha za mavazi hayo zilipokuwa zimebandikwa, alikiri kwamba yalikuwa mavazi mazuri mno.
Kiingilio kilikuwa kikubwa lakini watu walijazana na wengine kukosa kabisa nafasi, matangazo yaliyokuwa yametangazwa kwa kipindi kifupi yalisaidia sana, kila mtu akawa na hamu ya kutaka kuangalia jinsi ubunifu huo utakavyokuwa.
Elizabeth na Rasheed walipofika ukumbini hapo, msichana huyo hakuamini alichokiona, idadi kubwa ya watu waliokuwa mahali hapo walimshangaza, hakutegemea kukuta idadi kubwa ya watu kama ilivyokuwa.
Alipoingia, watu wakaanza kupiga makofi kwa shangwe, walikuwa wakimkaribisha ukumbini hapo. Wengi walimfahamu, alikuwa msichana aliyekuwa na fedha kuliko wanawake wote barani Afrika.
Kitendo cha kutangulizana na Rasheed ukumbini hapo kikawapagawisha watu zaidi, hawakuamini kuwaona wawili hao wakiwa mahali hapo pamoja. Waandishi wa habari waliokuwa ukumbini hapo, kama kawaida yao hawakubaki nyuma, wakaanza kupiga picha kila kitu kilichotokea.
“Siamini! Nashukuru sana,” alisema Elizabeth.
“Asante, ila usijali sana, nimefanya hivi kwa ajili yako, nataka ufikie utrilionea zaidi ambao kila siku umekuwa ukiuhitaji,” alisema Rasheed.
Usiku wa siku hiyo, kila kitu kikaenda kama ilivyotakiwa, watu wengi walivutiwa na mavazi yale kiasi kwamba hawakutaka kusubiri mpaka yatakapouzwa, wakahitaji mavazi hayo yaanze kuuzwa humohumo ukimbini kitu kilichofanyika kwa haraka sana na hivyo kila vazi kuuzwa kwa dola mia tatu.
“Utakwenda kuwa trilionea mkubwa, niamini,” alisisitiza Rasheed.
“Naamini hilo ila bado ninahitaji msaada wako!”
“Usijali, nitakusaidia mpaka utakapokamilisha ndoto zako.”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, hata Elizabeth aliporudi nchini Tanzania bado aliendelea kuwasiliana na Rasheed. Alimpenda mno, kila siku alihitaji kuwa naye karibu, hakujua ni kwa jinsi gani alimpenda mwanaume huyo lakini kila siku aliogopa kumwambia ukweli.
Sauti yake aliyokuwa akiisikia kwenye simu ilimtetemesha mno, kila wakati alitamani kuisikia kwani ilizitetemesha ngoma za masikio yake ipasavyo. Akawa akiugua moyoni, hofu ilimjaa, hakuwa na jinsi, kama ambavyo Rasheed alivyoonekana kutokujali uhusiano wa kimapenzi, basi naye akamchukulia hivyohivyo.
“Nitaweza kweli kuvumilia? Mmmh! Ngoja nione,” alisema Elizabeth.
Je, kiliendelea nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/