×

Wananchi Waombwa Kujitolea Kuchangia Damu Hospitali ya Sengerema

Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema (DDH) mkoani Mwanza inakabiliwa na upungufu wa uniti 12 za damu kwa siku hali inayofanya kuazima damu kutoka hospitali ya Nzera na Nyang’wale zilizopo mkoani Geita ili kunusuru maisha ya wagonjwa.
Akizungumza  wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo maalumu la uchangiaji damu lililojengwa katika hospitali hiyo kwa shilingi million 24, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Marie Jose alisema wastani wa uniti 17 za damu zinahitajika kila siku, akidai zinazopatikana ni uniti tano pekee hivyo kufanya upungufu kuwa uniti 12 za damu.
“Hospitali yetu inakabiliwa na uhaba  wa damu jambo ambalo linatufanya kuazima damu kutoka hospitali zingine mkoani geita ili kutusaidia kuwahudumia wagonjwa wetu, tunahitaji uniti 17 kwa siku lakini tunapata uniti 5 tu hivyo kufanya tuwe na upungufu wa uniti 12 ili kutosheleza mahitaji ya hospitali yetu kila siku”
Hivyo tunalazimika kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo maadhimisho ya siku ya wagonjwa duniani kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu niombe wananchi wawe na tabia ya  kujitolea kuchangia damu ili kunusuru maisha ya ndugu,jamaa na  marafiki zetu ”alisema Dk Merie
Aidha alisema wananchi watakao changia damu kwa hiari watapewa matibabu ya wagonjwa wa nje (OPD) bila malipo ili kutoa motisha wa watu kujitokeza kuchangia damu.
Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama katika hospitali hiyo, Elias Khamis alisema katika hospitali hiyo inayohudumia wastani wa wagonjwa 300 kwa siku inahitaji damu nyingi hivyo kukamilika kwa jengo hilo litakuwa msaada mkubwa kwa watu kujitokeza kuchangia damu na kupunguza uhaba uliopo hivi sasa.
“Kupitia zoezi hili la leo la uzinduzi wa jengo tumefanikiwa kupata uniti 35 za damu, kiasi hiki kitasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa kwa siku mbili tu”alisema Khamis
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Sengerema Antony Getere alisema licha ya kuwa na Hospitali ya Serikali katika wilaya hiyo lakini Hospitali ya DDH inatumika kama hospitali ya rufaa kutokana na huduma bora inayotolewa katika hospitali hiyo.
Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Padri Elias Masolwa aliwaambia wananchi kuwa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeridhia ombi la kuanzishwa kwa kitengo maalumu cha uchangiaji damu salama kwenye hospitali hiyo kutokana na mahitaji yaliyopo.
“Wananchi tunawaomba wajitokeze kwa wingi kuchangia damu huenda na wewe unayechangia leo, kesho utahitaji kuchangiwa na kwa kuzingatia kwamba tumeshapewa muongozo kwamba ukichangia utapewa huduma bure,”alisema Padri Masolwa.

Leave a Comment