
Makamu wa Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameungana na Watanzania kushiriki Siku ya Maombi na Dua ya kuliombea Taifa katika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo April 22, 2024.
Maombi hayo yanafanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali huki Kauli mbiu ikisema “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa letu”
“Uchumi wa Taifa letu limeendelea kupiga hatua katika sekta mbalimbali na kuboresha maisha ya Watanzania huduma za kijamii zimeendelea kuboreshwa ikiwemo katika sekta ya Elimu,Afya,Umeme,maji Uboreshaji wa barabara na ustawi wa jamii kwa ujumla pamoja na kuhakikisha usalama wa Wananchi lakini pia usalama wa Taifa letu,” amesema Dkt.Mpango.
Amesema tangu Muungano ulipoasisiwa mwaka 1964 umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo changamoto mbalimbali za Muungano zimekuwa zikitatuliwa kupitia mazungumzo ya pamoja na hivyo kujenga maelewano na mshikamano katika Taifa. Amesema mafanikio hayo ni kutokana na udugu na ushirikiano wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano uliokuwepo tangu zamani na nia ya dhati ya kujenga nchi na jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Amewasihi wananchi kuendelea kuenzi na kudumisha tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano, utu, haki, heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia.
Amesema wakati ikitimia miaka 60 ya Muungano, bado ni muhimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kasi ya maendeleo, kukuza ustawi wa jamii na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Taifa. Halikadhalika amewasihi watanzania wote kwa pamoja kwa kuongozwa na viongozi wa dini, Serikali, wazazi, walezi na walimu kuwajibika kuendelea kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika Taifa unaopelekea kuongezeka kwa matendo yanayokiuka mila na desturi za Kitanzania ikiwemo uhalifu, ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na mengineyo ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu.
Aidha Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuchukua hatua katika kudhibiti uhalifu na ufujaji wa fedha za umma na amewataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika pale uovu unapofanyika katika jamii ili hatua ziweze kuchukuliwa ,ametoa wito kwa Mihimili yote kufanya kazi kwa ushirikiano kwa manufaa ya nchi na watu wake amewasihi Watanzania kutumikia nchi kwa haki uadilifu na uzalendo.