×

Mashindano ya CAF African Schools Football Championship Kutimua Vumbi Zanzibar

Msimu wa pili wa fainali za mashindano makubwa zaidi ya mpira wa miguu kwa wanafunzi Africa, CAF African Schools Football Championship yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Mei 21 hadi Mei 24, 2024 katika Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Rais wa CAF, Dkt. Motsepe na idadi ya magwiji wa soka wa Afrika watahudhuria fainali hizo zitakazojumuisha washindi kutoka katika kanda za soka barani Afrika.

Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Shule za Afrika ya CAF yanashirikisha wavulana na wasichana walio chini ya umri wa miaka 15 na ni ya kwanza kwa soka duniani, likiwa ni wazo la Dkt. Motsepe katika maono yake ya kuwekeza katika soka la vijana wa Afrika.

Mashindano ya mwaka huu yana ongezeko la asilimia 40 za ushiriki ambapo kuanzia hatua za awali, wavulana na wasichana wa Kiafrika wapatao 804,480 kutoka shule 28,862 katika nchi 44 wanashiriki katika mashindano hayo.
Pamoja na jukwaa lake la kuwapa vijana nafasi ya kushindana kimataifa, mashindano haya yana programu ya kujenga uwezo inayowapa wanafunzi, makocha na waelimishaji ujuzi wa kipekee wa kujenga uwezo.

Katika Michezo ya Kanda, CAF imezindua programu mbalimbali za kujenga uwezo ambazo zilijumuisha Mpango wa Waandishi Vijana, Mpango wa Waamuzi Vijana, Mpango wa Maafisa wa Matibabu Vijana, Kozi ya Ukocha ya Leseni D ya CAF, pamoja na warsha za Ulinzi za CAF.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, fainali za Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Shule za Afrika ya CAF zinatarajiwa kuhudhuriwa na baadhi ya Magwiji wa CAF ili kuwasaidia kuhamasisha na kuwatia moyo wachezaji chipukizi.

Washindi wa mashindano ya wavulana na wasichana watapata kila mmoja zawadi ya dola za Kimarekani 300,000, washindi wa pili wakipata dola 200,000 kila mmoja, wakati washindi wa tatu watapata dola 150,000 kila mmoja, shukrani kwa ushirikiano wa CAF na Taasisi ya Motsepe kwa ajili ya kutumika kwa miradi ya maendeleo ndani ya shule.

Leave a Comment