
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amempa siku 14 Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha amewaondoa watu wote waliovamia ardhi inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mtaa wa Malela, Kata ya Toangoma Dar es Salaam.
Silaa amesema hayo Juni 5, 2024 katika Mtaa wa Malela Toangoma mara baada ya kuwakamata watuhumiwa sugu wanne wanaodaiwa kuwatapeli wananchi na kuwauzia ardhi, baada ya NSSF kuweka mtego uliofanikisha kutiwa nguvuni kwa watuhumiwa hao.

Amesema kuanzia sasa anapiga marufuku Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kujihusisha na mauzo ya ardhi pamoja na nyaraka za Serikali za mitaa kutumika kuuzia viwanja na kuwa hivi sasa Wizara ya Ardhi inafanya marekebisho ya GN ya mwaka 2021, inayotoa nyaraka zinazotumika katika mauzo ya ardhi ambapo wanatarajia kutoa nyaraka mpya za kuuza maeneo nchini.
“Watu wa Serikali za Mitaa wakae mbali na shughuli za ardhi kwa hili watatusamehe nipo makini sana na masuala ya ardhi pamoja na utapeli wa ardhi unaoendelea,” amesema Mhe. Silaa.

Aidha, amewaagiza Polisi kuwakamata watuhumiwa hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria huku akimuagiza Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) kufanya operesheni maalumu katika eneo hilo ili kuwakamata watuhumiwa wengine na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Nataka niwapongeze wenzetu wa NSSF kwa kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hawa ambao wamekuwa wakifanya uhalifu wa kuuza maeneo ya NSSF na kuwadhulumu wananchi,” amesema Mhe. Silaa.
Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Malela, Oswin Mkinga amewashukuru NSSF kwa kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuwa maeneo hayo yanamilikiwa na NSSF na ni sehemu ya mradi wa viwanja 20,000 vya Toangoma ambavyo vilinunuliwa kwa utaratibu wa fidia mwaka 2000.