
UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa utafanyia kazi makosa yaliyopita ili kurejea kwenye ubora wao kwa kuwa nyakati ambazo wamepita zimewaumiza.
Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda imegotea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69.
Imepishana na taji la ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika na inakwenda kushuhudia bingwa mpya wa CRDB Federation Cup ambaye ni Yanga.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa nyakati ambazo wamepitia ni ngumu na hazijawafurahisha hivyo wanapambana kurejea kwenye ubora.
“Hatujafurahi kuwa hapa na tumekuwa na huzuni kwa kuwa tumepoteza kila kitu ambacho tulikuwa tunakipigania kwenye msimu ulioisha.
“Yote kwa yote yaliyopita tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuwa bora wakati ujao mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”
Stori na Lunyamadzo Mlyuka, GPL