
Treni moja ya mizigo imegongana na nyingine ya abiria kwenye jimbo la mashariki mwa India la West Bengal mapema Jumatatu, na kuuwa takriban watu 8, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Mkuu wa mawaziri wa jimbo hilo Mamata Banerjee, kupitia ujumbe wa X amesema kuwa madaktari, timu za uokozi pamoja na maghari ya dharura, wapo kwenye shughuli za ukokozi kwenye eneo la tukio, ambalo ni karibu na wilaya ya kitalii ya Darjeeling, karibu na milima ya Himalaya.
Msemaji wa kampuni ya reli ya Northeast Sabyasachi De, amesema kuwa watu watatu miongoni mwa 8 waliouwawa ni wafanyakazi wa reli. Takriban wengine 25 wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo karibu na kituo cha treni cha New Jalpaiguri. Vituo vya televisheni vimeonyesha treni moja ikigonga nyingine upande wa nyuma na kusababisha behewa lake moja kugeukia upande wa juu.
Mamlaka za reli zimeambia vyombo vya habari kwamba ajali hiyo imesababishwa na treni ya mizigo ambayo haikusimama ilipohitajika. Mabehewa kadhaa kutoka kwenye treni ya abiria pia yanasemekana kuondoka kwenye njia ya reli.