
Kufuatia Kiliniki ya matibabu yaliyotolewa bure kwenye kambi ya Madaktari Bingwa na Mabingwa Wabobezi iliyofanyika kwa siku 7, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha, jumla ya wagonjwa 32,136 sawa na wastani wa wagonjwa 4,598 kwa siku, wamepatiwa huduma za matibabu, vipimo, dawa na vifaa tiba.
Taarifa hiyo imetolewa na Mganga Mkuu Mkoa wa Arusha, Dkt. Charle Mkombachepa, kwa waandishi wa habari wakati wa kufunga rasmi Kambi hiyo Julai 01, 2024 ikiwa ni siku ya nane kati ya siku 7 zilizopangwa kukamilisha kambi hiyo.
Dkt. Mkombachepa amesema kuwa, kambi hiyo ilianza Juni 24 ikiwa na wahudumu wa afya 450, ikiwa na lengo la kuhudumia wagonjwa 7,000 kwa wastani wa wagonjwa 1,000 kwa siku, lakini kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi waliofika kupata huduma, ililazimika kuongea watoa huduma na kufikia 550, walioweza kufanikisha kuhudumia wagonjwa hao 32,136.
Aidha ameainisha idadi hiyo ya wagonjwa waliweza kupata huduma ambazo wananchi wenye kipato cha chini wasingeweza kumudu gharama za vipimo hivyo, wanawake walikuwa 19,546 sawa na 60.7%, wanaume 12,640 sawa na 39.3% na watoto 4,616 sawa na 14.3%,
Amefafanua kuwa, pamoja na huduma zilizotolewa za vipimo wagonjwa 20 walipimwa kipimo cha RMI, wagonjwa 180 walifanyiwa kipimo cha CT – Scan, wagonjwa 1,820 walipewa rufaa kwenda hospitali ya Mount Meru ambapo 14 tayari wamefanyiwa pasuaji huku wagonjwa 31 wakiwa kwenye ratiba ya upasuaji, na kuongeza kuwa wagonjwa 170 wamepewa rufaa ya kwenda hospitali nyingine za rufaa wagonjwa 265 JCKI, wagonjwa 69 MOI, wagonjwa 20 Hospitali ya Taifa Muhimbili, wagonjwa 2 Benjamin Mkapa na wagonjwa 2 hospitali ya Mirembe Dodoma.
Hata hivya, amempongeza na kumsukuru Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda aliyebeba maono hayo yakiwa na lengo la kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wasio na uwezo wa kupata huduma hizo kutokana na kipato duni na hatimaye utekelezaji wake umezaa matunda mema yaliyorejesha matumaini kwa wagonjwa wengi.
Amewashukuru wadau wote waliojitoa kwa hali na mali kukamilisha zoezi hilo muhimu wakiongozwa Mhe. na RaisDkt. Samia Suluhu.