×

Benki Ya TCB na Metro Life Waja na Ada Bima Pamoja na Kikoba Cha Kidijitali

Mkuu wa Kitego cha Bima wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Francis Kaaya.

Benki ya TCB kwa kushirikiana na Metro Life wamekuja na mpango maalum wa Ada Bima ambao utakuwa  mkombozi kwa mwanafunzi kufikia malengo yake Kielimu hata kama itatokea bahati mbaya ya kuondokewa na aliyekuwa akimsomesha au dharura nyingine yeyote inayohusiana na ulipaji wa ada.

Akizungumza na wanahabari leo kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Mkuu wa Kitego cha Bima wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Francis Kaaya amesema katika maonesho hayo ya kibiashara wao kwa kushirikiana na Metro Life wamekuja na bidhaa hiyo ya Ada Bima.

Maofisa wa TCB wakiwa tayari kuwahudumia wateja kama walivyokutwa kwenye banda lao kwenye Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa ya Sabasaba.

Kaaya amesema bima hiyo ni ya kwanza hapa nchini ambayo imekuja kuleta ufumbuzi kwa wateja wao husasan kwa walezi na wazazi iwapo kuna mzazi anamsomesha mtoto wake katika ngazi ya shule ya msingi, sekondari au chuo kikuu mzazi endapo atafariki au kupata ulemavu wa kudumu bima ile itahakikisha yule mwanafunzi anasoma mpaka kumaliza ile elimu iliyokusudiwa na mzazi au mlezi. Alimaliza kusema Kaaya.

Afisa wa Huduma za Kidijitali wa TCB alipokuwa akizungumzia Kikoba cha Kidijitali

Kwa upande wake Afisa wa Huduma za Kidijitali wa TCB, alizungumzia huduma ya Kikoba cha kidijitali ambayo inatolewa na Tanzania Commercial Bank kwa kushirikiana na mitandao ya simu ambayo ni Vodacom, Tigo, Airtel pamoja na Halotel na kusema lengo ni kuviingiza vikundi vya kwenye Kikoba hicho cha kidijitali.

Afisa huyo amesema huduma hiyo inawahakikisha vikundi hivyo huduma salama na ya uhakika na kueleza kuwa huduma hiyo inakuwa ya uwazi kwa wanakikundi ambapo kila mwanakikoba atakuwa akijua salio la kikundi na mambo mengine ikiwemo miamala inayofanywa na mwanakikundi yeyote.

Afisa huyo alimalizia kwa kusema kikubwa zaidi katika kikoba hicho fedha hizo zinakuwa na usalama wa hali ya juu kwakuwa fedha hizo zinakwenda kutunzwa kwenye benki ya TCB ambayo ni benki ya serikali inayoendeshwa kiuhakika kabisa.

Leave a Comment