
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kufanya kazi na Donald Trump iwapo atachaguliwa tena kuwa rais wa Marekani itakuwa “kibarua kigumu, lakini sisi pia ni wachapakazi”.
Zelensky alisema yuko tayari kufanya kazi na yeyote aliye madarakani nchini Marekani.
Siku chache zilizopita, Trump alimtangaza Seneta wa Ohio JD Vance kama mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa Novemba. Vance mwenye umri wa miaka 39 hapo awali alisema kwa njia moja au nyingine hajali kinachotokea Ukraine.
Uteuzi huo umeibua upya hofu kwamba ahadi ya Marekani kwa Ukraine inaweza isitimie iwapo Trump atarejeshwa Ikulu katika uchaguzi wa Novemba.
“Labda haelewi kinachoendelea Ukraine, hivyo basi inabidi tushirikiane na Marekani,” Bw Zelensky
Kiongozi huyo wa Ukraine yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC), ambapo alitoa hotuba yake Alhamisi mchana.
EPC, ambayo inajumuisha wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya pamoja na wasio wanachama 20 kama Uingereza, ni jukwaa la ushirikiano usio rasmi.
Zelensky hapo awali alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ambaye ameapa kusimama na Ukraine kwa “muda wote ambao tutahitajika kufanya hivyo “na amejitolea kutumia £3bn kama msaada kwa nchi hiyo.
Alisema anatumai muda wa Bw Starmer ungeashiria enzi “maalum” katika sera za kigeni za Uingereza.