Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David silinde (Mb), ameshiriki katika Kongamano la Vijana na Wanawake kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane, tarehe 03 agosti, 2024 katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Mhe. Silinde ametoa wito kwa vijana na wanawake kuchangamkia fursa zilipo na zitakazoendelea kutokea katika Sekta ya Kilimo ili kufikia malengo yaliyowekwa na kuzitaka Wizara, Mashirika ya Maendeleo na Taasisi Binafsi kushirikiana katika kukuza Sekta kwa kuwa ni chachu ya maendeleo ya Taifa.

“Wito wangu kwa vijana, wanawake na wananchi mliofanikiwa kuona bunifu, huduma, teknolojia mbalimbali zilizooneshwa katika maonesho haya mkatumie elimu na maarifa mliyoyapata kwa lengo la kujiletea mapinduzi halisi katika kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao yetu ya kilimo” ameeleza Mhe. Silinde.

Pia Mhe. Silinde amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya juhudi mbalimbali zenye malengo ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ikiwa ni ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana kupitia Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tommorow -BBT) ambayo inatekelezwa nchi nzima kwa lengo la kuwavutia vijana kuwekeza katika kilimo kwa kuwawezesha kupata ardhi yenye miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mikopo ya riba nafuu na kuwaunganisha na masoko.
