ILIPOISHIA
Nikaingia na kutulia katika kiti cha dirishani, macho yangu bado yalikuwa yakimwangalia Mudi aliyekuwa nje. Kwa kumwangalia haraka alionekana kuwa wa kawaida lakini ukweli ni kwamba alikuwa mtu mwenye majonzi sana, kila aliponitupia jicho dirishani, alitamani kuniambia nirudi niishi naye.
“Nitarudi na kukusaidia Mudi, hata iwe vipi, nitarudi kulipa fadhila,” nilijisemea huku basi likiwashwa na safari ya kuelekea Ruaha kisha Morogoro Mjini kuanza.ENDELEA…
Siku hiyo nilikuwa na mawazo tele, nilikuwa njiani kuelekea Ruaha ambapo huko ningeteremka kisha kuchukua chumba na kesho yake kuendelea na safari ya kuitafuta Morogoro huku tukipita katika mbuga ya wanyama ya Mikumi.
Niliifikiria familia yetu, nilijua kwamba wazazi wangu walikuwa na mawazo tele, kitendo cha kutokuniona najua kiliibua maswali mengi juu ya mahali nilipokuwa lakini sikutaka kujali kwa kuamini kwamba wakati mwingine tunatakiwa kufanya maamuzi pasipo kuwasikiliza wazazi, kwani kama utawasikiliza, unaweza usifanikiwe hata kidogo.
Safari ya kutoka Ifakara kwenda Ruaha ilikuwa ndefu sana, njiani nililala na kulala, kila nilipoamka bado tulikuwa njiani. Nakumbuka siku hiyo tulitumia saa tano njiani, nilipofika Ruaha, sikutaka kuunganisha safari japokuwa kulikuwa na magari ya kwenda Morogoro, nikaenda kwenye nyumba ya wageni kupumzika.
Huko, hata usingizi haukunipata, nilikuwa na mwazo tele, wakati mwingine nilimfikiria Mudi, alionekana kuwa mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ambaye hakutaka niondoke mikononi mwake lakini kutokana na kunikuta nikiwa safarini, hakuwa na budi kuniacha.
“Nikuletee nini dada?” aliniuliza dada wa mapokezi baada ya kumwambia kwamba nilihitaji chakula.
“Niletee chipsi kama zipo…” nilimwambia japokuwa sikuwa hata na hamu ya kula.
Nikaondoka na kuelekea chumbani, baada ya dakika kadhaa, dada yule akaja chumbani na kuniletea chakula hicho. Hata hamu ya kukila sikuwa nayo zaidi ya kukishikashika kisha kukiweka pembeni.
Maneno ya baba ya kunikataza kwenda Dar yakaanza kujirudia kichwani mwangu. Kwa kweli yalinigusa lakini sikuwa na jinsi, iwe isiwe ilikuwa ni lazima niondoke na kuelekea huko na muda huo ndiyo nilikuwa njiani.
Usiku huo nikalala hapohapo na kesho asubuhi kuanza safari ya kuelekea Morogoro Mjini. Safari ilikuwa ndefu sana ila baada ya saa kadhaa tukafanikiwa kuingia Msamvu ambapo nikateremka, kabla ya kuondoka, kwanza nikaanza kuangalia kila kona.
Sikuwa nimewahi kufika mjini, kitendo cha kuona mazingira mazuri tofauti na kule kijijini nilipokulia, hakika ilinishangaza sana, nilipaona pale Morogoro Mjini kuwa sehemu nzuri sana, sikuwahi kuona maghorofa, kwa mara ya kwanza niliyaona, mambo mengi yaliyoonekana mbele yangu yalinishangaza mno.
“Dada unataka kwenda wapi?” aliniuliza mwanaume mmoja.
“Dar…” nilimjibu kwa kifupi.
“Mbona upo hapa sasa, twende, magari yale kule,” aliniambia mwanaume huyo.
“Kiasi gani?”
“Elfu kumi, unayo?”
“Ndiyo!”
“Basi twende…”
Mwanaume yule akachukua kibegi changu na kuanza kuelekea ndani ya basi moja, sikumbuki liliitwaje. Nikaingia ndani, akanipa mzigo wangu kisha kutulia kitini. Sikuwa nikiamini kilichokuwa kikiendelea, eti Zakia mimi, leo hii nilikuwa njiani kuelekea Dar. Safari ikaanza.
Kumbuka kwamba sikuwa na ndugu yeyote ndani ya Jiji la Dar es Salaam, nilikuwa nikienda mimi kama mimi, sikujua ningefikia wapi lakini hamu yangu ilikuwa ni kufika ndani ya jiji hilo tu. Njiani, sikutaka kulala, nilikuwa macho japokuwa nilichoka sana, nilitaka kuona huko mwanzomwanzo wa jiji hilo kulionekanaje.
“Hivi Dar kuzuri?” nilijikuta nikimuuliza mwanamke niliyekuwa naye.
“Ndiyo! Kwani hujawahi kufika?”
“Hapana kwa kweli…”
“Una ndugu huko?”
“Hapana!”
“Eeeh! Sasa unakwenda kufanya nini?”
“Nakwenda kutafuta utajiri!” nilimwambia yule mama, kwa mbali akaonekana kushangaa.
“Unakwenda kutafuta utajiri?” aliuliza kwa mshtuko.
“Ndiyo!”
Hakuuficha mshangao wake, aliniangalia kwa macho yaliyoonesha kuwa na maswali mengi mno, sikujua alijiuliza nini lakini hata kwa kuniangalia usoni, aligundua kwamba nilimaanisha nilichokuwa nikikisema kwamba nilikwenda Dar kutafuta utajiri tu.
Hakutaka kuniuliza swali jingine tena, akanyamaza na kuendelea na mambo yake huku nikipata muda zaidi wa kuangalia dirishani. Baada ya saa moja na nusu, nikahisi kwamba ndiyo nilikuwa nikiingia ndani ya jiji hilo, nyumba nzuri zilianza kuonekana, hisia zangu zikaniambia kwamba tayari tulikuwa tukiingia ndani ya jiji hilo.
“Ndiyo tumefika?” nilimuuliza baada ya ukimya wa muda mrefu.
“Ndiyo! Ila tunaelekea Ubungo, hapa panaitwa Kibamba…” aliniambia.
Japokuwa sikuwa nikipafahamu huko na wala kufika sikuwahi lakini nilikuwa na hamu kubwa ya kuliona jiji hilo. Kipindi cha nyuma nilipokuwa kijijini, kila mtu alitaka kwenda huko, hawakujali kama walikuwa na ndugu au la, walichokitaka ni kujiona wanaingia ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kufanya biashara kwa kuamini watafanikiwa.
Baada ya dakika arobaini, basi likaanza kuingia ndani ya kituo kikubwa cha Ubungo, huko, idadi kubwa ya watu ilinishangaza, haikuwa kama Morogoro, watu walionekana kuwa wengi huku wengi wao wakionekana kuwa bize wakifanya mambo yao.
Niliteremka na mwanamke yule kuondoka, sikuwa na pa kwenda, begi langu mikononi, kwa sababu humo kulikuwa na watu wengi, wa rika zote tena mbele nikiona kuna mikeka, nikasema pia ua, ilikuwa ni lazima na mimi niishi humohumo, hata kwenda huko nje, sikutaka kabisa, kama kula, nitakula humohumo, kama kufanya biashara, acha nifanye humohumo, ila kutoka ndani ya kituo cha Ubungo, nisingeweza, kwani hata kama ningetoka, ningekwenda wapi? Sikuwa na sehemu, hivyo kuishi humo niliona kuwa suluhisho. Na humo ndimo ningepata huo utajiri.
Dada kaamua huyo