×

Ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa Ruangwa, Yazoa Wanachama Wapya Wa CUF na ACT Wazalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Namikulo wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi, Agosti 23, 2024.    

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee baada ya kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Namikulo wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na ACT Wazalendo waliovihama vyama hivyo na kujiunga na CCM baada ya Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Namikulo wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi baada ya kuzungumza nao katika kijiji cha Namikulo wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi, Agosti 23, 2024.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa ameshuhudia wanachama 24 wa vyama vya CUF na ACT-Wazalendo wakirejea CCM ndani ya siku mbili.

Mheshimiwa Majaliwa alishuhudia wanachama hao wakikabidhi kadi zao kwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Abbas Mkwenda (Agosti 23 na 24, 2024) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Mtondo (Kata ya Nambilanje) na Namikulo (Kata ya Chunyu), wilayani Ruangwa, Lindi ambako alifanya ziara ya jimboni kwake.

Katika kijiji cha Mtondo, wanachama tisa wa CUF walirejesha kadi zao wakiongozwa na Mzee Bakari Abdallah Nanyambo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CUF Kata ya Nambilanje. Wengine ni Abdallah Ally Manjawila, Bakari Ally Nyanga, Bakari Abdallah Nampota, Mwanahawa Abdallah Komaje, Zaituni Omary Mitachi, Mwanahawa Rashid Chomwingo, Somoe Omary Mkupete na Amina Musa Pachela.

Katika kijiji cha Namikulo, wanachama watano wa ACT-Wazalendo walikabidhi kadi zao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Kata ya Chunyu, Bw. Rashid Ibrahim Nakotyo. Wengine kutoka chama hicho ni Jafari Ali Namkwacha, Maulid Juma Mbanda, Mwajibu Saidi Baluya na Sefu Salum Makukuta.

Wengine 10 waliohama kutoka CUF ni Juma Abdalla Ching’oma (Mwenyekiti wa Kata), Said A. Mnunguye, Mohamed Selemani Lipei, Zena Rajabu Kabanda, Mohamed Mhumbila, Ally Mohamed Maluva, Abdalla M. Mbandula, Mwanaidi Saidi Mpingo, Idi Abdalla Matwani na Said Juma Mkomole.

Akizungumza baada ya kupokewa, Mzee Bakari Abdallah Nanyambo alisema ana uzoefu wa miaka 31 kwenye mageuzi na kwa sehemu kubwa alikuwa meneja wa kampeni kwa hiyo yuko tayari kutumia uzoefu wake akiwa ndani ya CCM.

Leave a Comment