
MGOMBEA urais wa Republican nchini Marekani Donald Trump amechuana na mpinzani wake Kamala Harris wa Democratic katika mdahalo wa urais uliofanyika usiku wa kuamkia leo Septemba 11, 2024 nchini humo.
Wagombea hao wawili wameonekana wakishutumiana kwa kila mmoja wao kusema uwongo katika masuala kadhaa ya msingi.
Kwa mfano, katika suala la uchumi, Makamu wa Rais Kamala Harris amejibu kwa kumshambulia Trump akielekeza lawama kwa utawala wake.
“Donald Trump alituacha na ukosefu mbaya zaidi wa ajira tangu kutokea kwa mdororo mkubwa wa kiuchumi nchini Marekani,” amesema.
“Tulichofanya ni kusafisha uchafu wa Donald Trump,” Harris ameongeza.
Trump alijibu, akisema maprofesa wa uchumi wameuchukuliwa mpango wake wa kiuchumi kuwa wa kipekee, na mzuri zaidi.
Katika suala la uhamiaji, Trump ametoa madai yasiyo na msingi kwamba wahamiaji wanakula wanyama katika eneo la Springfield, Ohio.
“Wanakula mbwa Wanakula wanyama wa nyumbani wa watu wanaoishi huko,” Trump alisema.
Hata hivyo, muongozaji wa mdahalo huo David Muir alibainisha kuwa meneja wa jiji huko Springfield amesema hakuna ushahidi wa dai hilo.