
UTATA umeibuka kuhusu kifo cha Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ulyankulu, Kaliua mkoani Tabora, Dk. Disma Chami, aliyetoweka siku 11 zilizopita baada ya mwili wake kukutwa porini.
Mwili wa daktari huyo umekutwa katika pori huko Kaliua, huku pembeni kukiwa na dawa mbalimbali za hospitalini.
Taarifa zilizosambaa mitandaoni mapema jana, zilieleza kuwa Dk. Chami aliondoka nyumbani kwake Septemba 4, mwaka huu, akimuaga mke wake kuwa angerejea kesho yake.
Hata hivyo, hakurejea na alipotafutwa kupitia simu yake hakupatikana na ilipofika Jumatano ya wiki hii (Septemba 11) ilipatikana lakini kila alipopigiwa hakupokea.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa baada ya kutokupokea simu muda mrefu, inadaiwa kuwa alituma ujumbe mfupi kwa mke wake uliosomeka hivi, “Nisamehe sana, baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichokiacha pesa zote zipo CRDB bank, simamia watoto wasome kwaheri.”
