
Waasi wa Houthi wamedai kwamba walirusha kombora la masafa marefu kutoka Yemen kuelekea Uwanja wa Ndege wa Tel Aviv wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alipokuwa akitua na ndege nchini Israeli kwa lengo la kumuua ili kulipa kisasi cha kifo cha kiongozi wa Hezbollah, Sayyed Hassan Nasrallah.
Hata hivyo, kombora hilo lilinaswa na mifumo ya usalama wa anga ya Jeshi la Israel na kulipuliwa kabla halijafika lilikokusudiwa kufika na kusababisha mlipuko mkubwa.
Muda mfupi baada ya jaribio hilo, Netanyahu alitoa hotuba kwa taifa ambapo alitetea hatua za Israeli za kumuua kiongozi huyo wa Hezbollah na kueleza kuwa walikuwa ‘wamelipa kisasi’ kwa kifo cha Nasrallah, mtu aliyemwelezea kama ‘muuaji mkubwa’.
Akaongeza kuwa kifo cha kiongozi huyo wa Hezbollah ni mwanzo tu na kwamba kutakuwa na mashambulizi mengine kama hayo.
“Hakuna mahali popote Iran au Mashariki ya Kati ambapo mkono mrefu wa Israeli hauwezi kufika.”
Wakati akitoa hituba hiyo, king’ora cha hatari za anga kilikuwa kikisikika maeneo mbalimbali ya Israel hasa katika Jiji la Tel Aviv, kufuatia jaribio hilo la Houthi.