×

Kanisa Katoliki wakataa mchango wa Ruto, waonya dhidi ya kupiga siasa kanisani

Rais wa Kenya William Ruto

Baraza la Maaskofu wa Katoliki Kenya (KCCB) limekataa mchango wa Shilingi za Kenya milioni 5.6 (takriban Shilingi za Kitanzania milioni 104) uliotolewa na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, wakati wa ibada katika Kanisa Katoliki la Soweto siku ya Jumapili.

Askofu Mkuu wa Metropolitan, Philip Anyolo, kupitia taarifa yake siku ya Jumatatu, alisema fedha ambazo tayari zilipokelewa zitarejeshwa.

Rais Ruto alitoa KSh 600,000/TZS milioni 11.2 kwa ajili ya kwaya na KSh milioni 2/TZS milioni 37.5 kwa ujenzi wa nyumba ya ‘Father’, pamoja na ahadi ya KSh milioni 3/TZS milioni 56.2 zaidi kwa ajiili ya basi la parokia. Kwa upande wake, Gavana Sakaja alichangia KSh 200,000/TZS milioni 3.7.

“Wanasiasa wanakaribishwa sana kuhudhuria ibada Kanisani kwa ajili ya ustawi wa kiroho, lakini wanashauriwa kufanya hivyo kama waumini wa kawaida bila kutumia nafasi hiyo kwa maslahi ya kisiasa,” amesema Anyolo.

Amesisitiza umuhimu wa Kanisa kudumisha msimamo wa kutokuwapendelea wanasiasa ili kubaki mahali pa ustawi wa kiroho na msaada kwa jamii, pasipo na ushawishi wa kisiasa.

“Kulingana na maelekezo haya, na kwa kufuata Sheria ya Misaada ya Umma ya Mwaka 2024, Kifungu cha 10(2), inabainika kwamba mtu yeyote anayetoa au kupokea pesa au manufaa yoyote kwa njia ya kuchangisha misaada, iwe kwa uwazi au kwa njia ya moja kwa moja, anapaswa kuwa na kibali cha kuchangisha fedha kwa mujibu wa sheria hiyo,” amesema Anyolo.

Uamuzi huu unakuja kufuatia ukosoaji wa hivi karibuni kutoka kwa maaskofu wa Katoliki walioutuhumu serikali kwa ukosefu wa uadilifu na kushindwa kutekeleza wajibu muhimu, ikiwemo ulipaji wa madeni kwa watoa huduma muhimu.

WAZIRI AWESO AKAGUA TANKI la BOZA na MADANGA MRADI wa MIJI 28

Leave a Comment