
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe amewataka waombaji wote wa ajira za Afya kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuzingatia utaratibu uliowekwa kwenye tangazo, ambapo mfumo unawataka kuchagua hadi kituo watakachofanyia kazi kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye kanzi data ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Dkt. Grace ameyasema hayo akifungua mafunzo ya mpango wa uwekezaji wa huduma za Afya ya Mama na Mtoto (TMCHIP) yaliyofanyika mkoani Morogoro yakihusisha Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, Wahandisi majengo, Maafisa Ugavi, Maafisa Mipango, Wahasibu, PPRA,Waratibu wa Miradi, Makatibu wa Afya na Waganga wafawidhi kutoka katika mikoa 17 na Halmashauri 25 ambapo mradi huo umeanza kutekelezwa mwishoni mwa juma hili.

“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuomba kazi, wakishapata wanaanza kutuma maombi ya kubadilisha vituo vya kazi tofauti na walivyoomba awali, nataka niwaambie hatutapokea mabadiliko kwa sababu nafasi hizi za ajira zimezingatia mahitaji ya vituo husika, usipoenda tunabadilisha na kuweka mtu mwingine anaesubiri ajira” Dkt. Grace.
Dkt. Grace aliwakumbusha waombaji wa ajira wote kuwa mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 20.12.2024.
