Kufuatia tukio lililotokea siku ya Mwaka Mpya na kuzua gumzo kubwa la mwanaume aliyetambulika kwa jina la Matthew Livelsberger (37) kutoka Colorado nchini Marekani, kulipua gari aina ya Tesla Cybertruck nje ya Hoteli ya Trump, imebainika kwamba mwanaume huyo alituma meseji kwa ex wake, Alicia Arritt muda mfupi kabla ya kufanya tukio hilo.
Uchunguzi uliofanywa na FBI ndiyo uliobaini kuwepo kwa mawasiliano kati ya mwanaume huyo ambaye imebainika kuwa alikuwa ni mwanajeshi wa Marekani, ambapo aliwasiliana na mwanamke huyo muda mfupi kabla ya kutekeleza tukio hilo.
Baada ya FBI kumfuatilia mwanamke huyo, ndipo ilipobainika kuwa kumbe alikuwa ni ex wake na katika meseji alizokuwa anamtumia, alikuwa akijigamba kuhusu gari hilo alilokuwa amelikodi huku meseji moja ikisomeka: ‘Najihisi kama Batman’.
Aliendelea kujigamba kwa mpenzi wake huyo wa zamani kwamba Cybertruck aliyokodi ilikuwa ya kasi isiyo ya kawaida, ikimfanya ajisikie kama ‘Batman’ huku meseji nyingine zikisomeka: Nilikodisha Tesla Cybertruck. Ni poa sana. Najihisi kama Batman au Halo,” alisema akimaanisha video game maarufu.
Muda mfupi baadaye, Livelsberger alijipiga risasi akiwa ndani ya Tesla Cybertruck, gari hilo likiwaka moto karibu na hoteli ya Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump iliyopo Las Vegas.
Inazidi kuelezwa kuwa, ukiachana na kumtumia meseji Alicia, mwanaume huyo pia alituma meseji kwa wapenzi wake wa zamani wengine huku taarifa za ndani zilieleza kuwa mwanaume huyo alijipiga risasi zikiwa ni siku sita baada ya mkewe, Jennifer Davis kumwacha akimtuhumu kwamba alikuwa akimcheat.
Arritt amefichua mawasiliano hayo kwa kuonesha picha za skrini za mawasiliano yao ambapo kwa mujibu wa Arritt, Livelsberger alikuwa “kama mtoto aliyepata toy mpya baada ya kukodi Cybertruck iliyotumika katika mlipuko huo.
Wakati wa mawasiliano yao, Arritt alimwuliza Livelsberger kuhusu kasi ya gari hilo, naye alijibu kuwa ilikuwa ya “ajabu sana.” Katika mazungumzo hayo, Livelsberger pia alijigamba kuwa anatengeza drones katika kazi yake mpya.
Livelsberger na Arritt walikuwa na uhusiano kati ya mwaka 2018 na 2021.