Mamlaka nchini Marekani zinafanya uchunguzi kuhusu uhusiano wa safari za nje ya nchi kwenda Misri na Canada zilizofanywa na mtuhumiwa wa tukio la kigaidi la New Olreans lililosababisha vifo vya watu 15.
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limebaini kwamba, Shamsud-Din Jabbar, mwanajeshi mstaafu wa Marekani aliyejinasibu hadharani kuliunga mkono Kundi la Kigaidi la ISIL (ISIS) kwenye video alizopost mtandaoni kabla ya shambulio hilo, alisafiri kwenda Misri na Canada katika majira ya kiangazi ya mwaka 2023, afisa wa FBI alisema Jumapili.
“Maafisa wetu wanatafuta majibu kuhusu alikoenda, alikutana na nani, walizungumza nini na safari hizo zina uhusiano gani na matendo yake katika jiji letu,” Lyonel Myrthil, Afisa wa FBI New Orleans,” aliwaambia waandishi wa habari.
Inazidi kuelezwa kuwa Jabbar pia alifanya safari mbili za kwenda New Orleans, mwezi Oktoba na Novemba.